Jumatatu, Januari 18, 2016

SIMBACHAWENE AWASIMAMISHA KAZI WAKURUGENZI KIGOMA NA KATAVI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa George B. Simbachawene (Mb) amewasimamisha kazi Wakurugenzi Watendaji wa Manispaa za Kigoma, Mkoa wa Kigoma na Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi kwa tuhuma za kuridhia na kutekeleza maamuzi ambayo yamesababishia Serikali hasara na upotevu wa fedha.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Mhandisi Boniface Nyambele anakabiliwa na tuhuma ya uuzaji wa nyumba za Halmashauri bila kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo na bila kibali cha Waziri Mwenye Dhamana kama Sheria inavyo elekeza.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Ndugu Suleiman Lukanga ana kabiliwa na tuhuma za Ununuzi hewa wa gari la kusomba taka kwa kiasi cha shilingi milioni tisini na mbili na laki saba na elfu hamsini (92,750,000/=) na ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Kakese kiasi cha shilingi milioni mia mbili, tisini na nne (294,000,000/=).
Aidha, Mheshimiwa Waziri wa Nchi ameagiza nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma ikaimiwe na Mhandisi Sultan Imari Ndilowa ambaye ni Mkuu wa Idara ya Maji, Manispaa ya Kigoma, nafasi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda ikaimiwe na Ndugu Lauteri John Kanoni ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Waziri wa Nchi, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kote Nchini kuwa makini katika kutekeleza majukumu yao wafuate Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wote ambao watakiuka matakwa ya Sheria, Kanuni na Taratibu na kutoweka mbele maslahi ya Umma.

0 comments:

Chapisha Maoni