Kiungo wa kutumainiwa wa Yanga na timu ya taifa ya Rwanda amerejea kwenye timu yake ya Yanga baada ya kutimuliwa na uongozi huo kutokana na sababu za kinidhamu.
Leo January 17, 2016 Niyonzima ameomba radhi kwa wanachama, viongozi na wachezaji wenzake kwa kile ambacho kilitokea miezi michache iliyopita. Niyonzima ameshaomba radhi mbele ya waandishi wa habari na kwa sasa anasubiri taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa Yanga kuhusu suala kusamehewa kwake.
“Nitumie fursa hii kuwaomba radhi viongozi, wanachama, wachezaji wenzangu pamoja na mashabiki wa Yanga kutokana na yale yote yaliyopita nyuma. Mimi niliondoka kwenda kuichezea timu yangu ya taifa ya Rwanda lakini nilichelewa kurejea kwenye klabu yangu na hapo ndipo matatizo yalianza”, amesema Niyonzima.
“Kiukweli nilikosea kwasababu sikutoa taarifa kwa timu yangu na ikachukua uamuzi wa kunifukuza kwenye timu, lakini tumekaa chini na kuzungumza na uongozi na kufikia sehemu nzuri ndiyo maana mpaka sasa niko hapa”
“Nilistushwa na uamuzi ambao ulichukuliwa na klabu yangu kwasababu sikutarajia kitu kama hicho kingetokea, kiukweli nilikuwa surprised na niliumizwa na uamuzi huo lakini nashukuru mambo haya yamefikia hatua nzuri”.
Msemaji wa Yanga Jerry Muro amesema uongozi wa klabu yake unajipanga kutoa taarifa rasmi kuhusu suala la Niyonzima ambayo itahitimisha mjadala kuhusu kiungo huyo.
“Sisi kama uongozi wa Yanga, tunamshukuru Niyonzima kwa kuwa muungwana juu ya hili suala na kuamua kuja kwa uongozi wa Yanga na kuomba radhi kwa yote yaliyotokea”, amesema Muro.
“Niyonzima kwetu ni kama mtoto kwa hiyo uongozi umekaa na kuzungumza naye na utatoa taarifa rasmi hivi karibuni na kuhitimisha mjadala wa mchezaji huyo”.
Haruna Niyonzima alifungashiwa virago na uongozi wa Yanga kutokana na sababu za utovu wa nidhamu ambao umekuwa ukijirudia kila mara hasa kuchelewa kurudi pindi anapokweda nyumbani kwao kuitumikia timu yake ya taifa au anapokuwa kwenye mapumziko ya likizo.
Fahari News
Fahari News
0 comments:
Chapisha Maoni