Halmashauri ya jiji la Mbeya kupitia mkurugenzi wake dkt. Samwel Lazaro imewataka wafanyabiashara wote wa jijini hapa kutoa kodi, tozo na ushuru wanaopaswa kutoa ili kuiwezesha mamlaka ya halmashauri ya jiji kufanya kazi zake za kuwatumikia wananchi ipasavyo.
Mkurugenzi wa jiji amesema kuwa ili halmashauri iweze kutoa huduma za kijamii ipasavyo, basi ni vema wafanyabiashara wakaacha kukwepa kodi wanazopaswa kuzitoa.
Halmashauri ya jiji la Mbeya imefanikiwa kukusanya kiasi cha 24% pekee mpaka kufikia mwezi novemba kwaka 2015, 74% pungufu ya makadirio ya ukusanywaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2015-2016.
Akieleza mbele ya waandishi wa habari dkt. Lazaro amesema kuwa kati ya sababu kuu zilizosababisha upatikanaji wa mapato kwa kiasi hicho kidogo ni pamoja na ukwepaji kodi uliokithiri kwa wafanya biashara na kuongeza kuwa kiasi cha mapato yanayopatikana ndio kiasi cha utekelezwaji wa huduma za jamii zinazofikishwa kwa wananchi hivyo ili huduma za jamii ziwe timilifu lazima mapato yakusanywe ipasavyo kutoka katika vyanzo ikiwamo ushuru, tozo na kodi kutoka kwa wafanya biashara wakubwa na wadogo.
Pamoja na hayo, Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mbeya amesema kuwa serikali imeidhinisha kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 12 kwaajili ya uboreshaji wa miundombinu katika jiji la Mbeya ikiwa ni pamoja na uwekwaji wa taa za barabarani, ujenzi wa mifereji katika barabara, ujenzi wa njia za kuelekea katika makazi ya watu (access roads), ujenzi wa maghuba makuu mawili ya taka n.k ambapo hii ni katika barabara zote mpya zilizojengwa na halmashauri ya jiji la Mbeya ambazo zinaurefu wa km 23.
0 comments:
Chapisha Maoni