Raia wa Kuwait,
Hussain Ahmed Ally Mansour (34), amekamatwa na maofisa usalama na Jeshi
la Polisi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
kwa tuhuma za kutaka kusafirisha kenge hai 149 wenye thamani ya Sh.
milioni 6.33 kwenda nchini Kuwait.
Tukio hilo la kusafirisha wanyama hai ni la pili kutokea nchini, la
kwanza lilitokea mwaka 2010, baada ya twiga hai wanne waliosafirishwa
kwenda nje katika mazingira yenye utata na hivyo kuzua mjadala ndani na
nje ya nchi.
Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Hamis Seleman, alisema
mtuhumiwa huyo alikamatwa juzi saa 5:20 usiku akiwa ameficha kenge hao
kwenye mifuko midogo 15 ndani ya begi jeusi kwa lengo la kuwasafirisha
kwenda Kuwait kupitia Dubai kwa ndege ya Shirika la Emirates.
Alisema mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa na hati ya kusafiria yenye
namba 003870237, alibainika akitaka kusafirisha kenge hao baada ya
vyombo vya usalama katika uwanja huo kufanya upekuzi wa mizigo kabla ya
abiria kuruhusiwa kuingia kwenye ndege.
Kamanda Seleman alisema baada ya kukamatwa, mtuhumiwa huyo
alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Uwanja wa Ndege Dar es Salaam
kwa ajili kuhojiwa ili hatua za kisheria zichukuliwe.
0 comments:
Chapisha Maoni