Jumanne, Oktoba 28, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA

Siku kama ya leo miaka 1429 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Muharram mwaka wa 7 Hijria, Mtume Muhammad SAW alianza kuwatumia barua rasmi wafalme wa tawala mbalimbali duniani kwa shabaha ya kuwalingania dini tukufu ya Uislamu. Baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani kati ya Mtume SAW na washirikina wa Makka huko Hudaibiya, Mtume Muhammad SAW alipata fursa ya kuwalingania dini ya Uislamu viongozi wa tawala kubwa duniani. Wanahistoria wanasema kuwa Mtume aliandika barua 12 hadi 26 kwa watawala mbalimbali katika kipindi hicho wakiwamo watawala wa Roma, Iran, Uhabeshi, Bahrain, Yemen na maeneo mengine. Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilionesha wazi kuwa dini ya Kiislamu inalingania haki kwa kutumia mantiki na hoja madhubuti.
Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita wanajeshi laki mbili wa Italia waliishambulia Ugiriki kwa amri ya Musolini, kiongozi wa serikali ya kifashisti ya nchi hiyo. Mashambulizi hayo yalifanywa wakati Vita vya Pili vya Dunia vilipokuwa vimepamba moto kwa kuchochewa na Ujerumani ya Kinazi, nchi muitifaki wa Italia huko Ulaya. Mashambulio ya Italia yalikabiliwa na mapambano makali ya wananchi wa Ugiriki na hatimaye yakashindwa.
Na miaka 66 iliyopita wakati wa vita vya kwanza kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu, wanajeshi wa utawala huo waliwaua kwa umati wakazi wa kijiji cha al Dawayima huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Wazayuni hao walivamia msikiti wa kijiji hicho na kuwauwa shahidi Waislamu 75 raia wa Palestina waliokuwa wakisali. Vilevile waliwaua kwa umati watu wa familia 35 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika pango moja nje ya kijiji hicho. Askari jeshi wa utawala haramu wa Israel walikisawazisha na ardhi kijiji hicho baada ya kuwaua kwa umati wakazi wake wote.

0 comments:

Chapisha Maoni