Kiungo mkongwe kutoka nchini Italia Andrea Pirlo amewataka
mashabiki wa klabu ya Liverpool kupunguza munkari dhidi ya mshambuliaji
Super Mario Barwuah Balotelli kutokana na kiwango anachokionyesha tangu
aliposajiliwa huko Anfield.
Pirlo ambaye ni kiungo wa klabu bingwa nchini Italia Juventus amesema
hakuna haja kwa mashabiki wa klabu ya Liverpool kumnyooshea vidole
mshambuliaji huyo na badala yake wanatakiwa kuwa wastahamilivu na
kutarajia mazuri kutoka kwake.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 37 amesema kwa kipindi cha miaka
kadhaa alimfahamu Balotelli na jambo kubwa alilolibaini kwa mshambulaiji
huyo ni kuhitaji kupewa nafasi na kuonyeshwa upendo katika jamii
inayoishi nae.
Amesema kinachokosekana kwa mashabiki wa Liverpool dhidi ya Mario
Balotelli, ni kukosekana kwa mapenzi baina ya pande hizo mbili na
mwishowe mambo yamekuwa yakienda mrama ndani na nje ya uwanja.
Amesema endapo Balotelli atapewa nafasi na kuonyeshwa upendo na kila
mmoja huko Anfiled atafanikisha azma ya kucheza soka safi na kufunga
mabao kama inavyohitajika na walio wengi.
Super Mario Barwuah Balotelli amecheza mara kadhaa na Andrea Pirlo
katika kikosi cha timu ya taifa ya Italia tangu mwaka 2010 na tayari
amecheza michezo 33 na kufunga mabao 12 akiwa na mabingwa hao wa dunia
wa mwaka 2006.
Balotelli alisajiliwa na klabu ya Liverpool majira ya kiangazi
akitokea nchini kwao Italia kwenye klabu ya AC Milan kwa ada ya uhamisho
wa paund million 16 na tayari ameshacheza michezo kumi akiwa na klabu
hiyo ya nchini Uingereza huku akifunga bao moja.
0 comments:
Chapisha Maoni