Familia ya Bwana Sata imesema kuwa Rais wa Zambia, Michael Sata, amefariki dunia akiwa na umri wa
miaka 77 katika hospitali ya London alikokuwa akitibiwa ugonjwa ambao
haujatajwa. Kifo chake kimetokea siku chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.
Mwanasiasa
huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya kuongoza
chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye
alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party
Democracy, kikiwa madarakani kwa miaka ishirini.
Michael Chilufya
Sata alizaliwa mwaka 1937 katika mji wa Mpika, eneo ambalo lilikuwa
wakati huo ni Northern Rhodesia. Muumini wa dini ya Kikristo ya
madhehebu ya Katoliki, alifanya kazi kama afisa polisi, mfanyakazi wa
reli na mwanachama wa chama cha wafanyakazi wakati wa utawala wa
kikoloni. Baada ya Zambia kupata uhuru wake, pia aliishi kipindi fulani
mjini London, akiwa mfanyakazi wa reli, na kurejea Zambia, akiwa na
kampuni ya teksi.
Akiwa mwenye sauti ya mkwaruzo yakiwa ni matokeo
ya kuvuta sigara kwa muda mrefu, Bwana Sata aliibuka katika siasa na
kupata umaarufu katika miaka ya 1980.
Haraka akapata sifa ya kuwa
gavana mwenye kuchapa kazi kwa bidii, wakati akiongoza jimbo la Lusaka
na mtu wa utekelezaji kwa vitendo.
Lakini pia alijulikana kama mtu
wa kutoa amri, mtu asiyeendekeza urafiki na mkali- na wapinzani wake
walisema jina alilopewa la bandia la "King Cobra" alikuwa anastahili
kuitwa hivyo.
Kwa mara ya kwanza alionekana kama mtu ambaye
angetekeleza ahadi za kupambana na rushwa na kupata ufumbuzi wa tatizo
la ajira na kuleta ustawi wa jamii. Lakini kipindi chake madarakani
kiligubikwa na kuuzima upinzani wa kisiasa na kudorora kwa uchumi.
Bwana Sata ni rais wa pili wa Zambia kufariki dunia akiwa madarakani.
0 comments:
Chapisha Maoni