Jumapili, Oktoba 26, 2014

DIAMOND AOMBA RADHI

Hatimaye msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdallah ‘Diamond Platinumz,’ ameliomba radhi Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kutumia magwanda ya kijeshi hilo bila kuwa na kibali.
Diamond amechukua hatua hiyo ikiwa ni siku chache tangu awe katika mazingira ya kubanwa na jeshi la Polisi nchini akiitwa kuhojiwa na kuachiwa mara kadhaa.
Katika mazingira hayo, Diamond aliamua kusalimisha magwanda hayo kabla ya kuandika barua kwa JWTZ, akiomba radhi kwa kufanya kitendo hicho. 
Nyota huyo wa muziki wa bongo flava, amejikuta katika sakata hilo baada ya kutinga katika shoo ya Serengeti Fiesta akivalia mavazi yanayofanana na sare za JWTZ.
Kwa mujibu wa mtu wa karibu wa Diamond, baada ya msanii huyo kubanwa kwa kuhojiwa mara kadhaa, Oktoba 22 alialazimika kuomba radhi akiwa makao makuu ya jeshi hilo.
Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo nakala yake imetupiwa katika mitandao ya kijamii, inasomeka hivi:
Mimi msanii wa muziki wa Kitanzania (Bongo fleva) Naseeb Abdallah maarufu kama ‘Diamond Platinumz’ naomba radhi kwa kosa nililolifanya la kutumia nguo za jeshi la Wananchi wa Tanzania nilizozivaa kwa dhumuni la kufanyia video ya nyimbo yangu siku ya tarehe 18/10/2014.
Natanguliza shukrani zangu na nina imani nitasamehewa na sitorudia tena kutumia nguo hizo
ilisema sehemu ya barua hiyo kwa JWTZ.
Sakata la msanii huyo na jeshi la Polisi, lilizua mjadala mzito huku wengine wakihoji siri ya ujasiri wa Diamond na wasanii wengine nchini kufanya hivyo.
Hii ni kutokana na msaniii Gwamaka Kaihula ‘Crazy GK’ kuwahi kukamatwa na kuhojiwa kwa kuvaa mavazi hayo ya jeshi katika wimbo wake wa ‘Simba wa Afrika’.
Naye Juma Kiroboto ‘Juma Nature’ aliwahi kupata adhabu ya kuvuliwa nguo hizo za jeshi wakati anapiga shoo katika moja ya matamasha hapa nchini na msanii Erick Msodoki ‘Young Killer’ aliwahi kuvuliwa alipokatiza katika eneo la JKT la Mwanza.

0 comments:

Chapisha Maoni