Ijumaa, Septemba 12, 2014

WATOTO ZAIDI YA 2,000,000 HUFA KWA MWAKA KUSINI MWA ASIA

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeeleza wasiwasi mkubwa ulionao kutokana na kuongezeka vifo vya watoto kusini mashariki mwa Asia. Taarifa ya UNICEF imesema kuwa, katika eneo la kusini mwa Asia kila mwaka zaidi ya watoto milioni mbili hupoteza maisha yao kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano. Ripoti ya UNICEF imebainisha kwamba, watoto hao hufariki duniani ilihali inawezekana kuzuia vifo vyao. Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umeeleza katika ripoti yake hiyo kwamba, licha ya kuweko kasi ya kukua uchumi na maendeleo makubwa yaliyopatikana kuhusiana na haki za watoto kusini mwa Asia, lakini bado watoto wa maeneo hayo wanataabika kwa mambo mbalimbali. Mkurugenzi wa UNICEF katika eneo la kusini mwa Asia amesema kuwa, asilimia 38 ya watoto wa eneo hilo wana matatizo makubwa ya lishe duni. Karin Hulshof ameeleza kuwa, eneo la kusini mwa Asia limegeuka na kuwa moja ya maeneo hatari duniani kwa akina mama wajawazito na kwamba, eneo hilo linashikilia nafasi ya pili duniani kwa idadi ya akina mama wanaopoteza maisha yao.

0 comments:

Chapisha Maoni