Alhamisi, Septemba 04, 2014

WANAWAKE IRINGA NA PESA

Wanawake Mkoani Iringa wametakiwa kuitumia mikopo kwa kazi ya uzalishaji mali ili kuondokana na utozwaji wa riba zitokanazo kwa kuchelewa na kushindwa kulipia mikopo hiyo. 
Akiwa katika uzinduzi wa tawi jipya la mfuko wa kusaidia wanawake wa Mama Bahati Foundation wilayani Mufindi, Mkuu wa wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa Dkt. Evelista Kalalu amesema asasi nyingi zimekuwa zikitoa mikopo kwa wananchi pasipo kutoa elimu ya uendeshaji wa mikopo hiyo kwa maendeleo ya familia zao na taifa kwa ujumla.Dkt. Kalalu ametoa wito kwa asasi mbalimbali zinazojishughulisha na utoaji wa mikopo kuwa na riba ndogo hali itakayopelekea maendeleo kwa wananchi ili waweze kunufaika na mikopo hiyo. 
Naye mkurugenzi wa mfuko huo Bw. Japhet Makau amesema lengo la mfuko huo ni kutoa mikopo ya fedha pamoja na vifaa vya umeme wa jua yenye liba ndogo kwa kila kikundi chenye wanachama zaidi ya watano ili kiweze kuwa na uwezo wa kukopa.
Mmoja wa wanachama wa mfuko huo ambaye pia ni mwenyekiti wa kikundi cha Njiapanda-Nyololo Wilaya ya Mufindi Bi.Leokadia Simfukwe amesema wanawake wengi wamekuwa hawajishughulishi na kazi za uzalishaji mali licha ya kupata elimu ya ujasilia mali.
Hata hivyo Mwenyekiti wa mfuko wa mama bahati foundation Padri Bernad Mtemela amesema wanawake ni nguzo ya familia hivyo wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii,uadilifu na uaminifu pamoja na kumtumikia Mungu ili waweze kufanikiwa katika kazi zao za kila siku.

0 comments:

Chapisha Maoni