Taarifa kutoka UKAWA: Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Tuligoma mbele ya Rais
Jakaya Kikwete kuruhusu wajumbe wao kurejea katika Bunge Maalumu la
Katiba, walipokutana katika kikao cha kusaka suluhu ya mkwamo wa
mchakato wa Katiba.Mkutano wa jana ulikuwa na sehemu mbili kuu, wa
kwanza ulifanyika katika Ikulu ya Kilimani, Dodoma ambako viongozi hao
walikutana na Rais Kikwete na mwingine katika Hoteli ya St. Gasper ambao
uliwashirikisha viongozi na maofisa wa vyama vilivyoshiriki bila Rais
Kikwete.Mkutano huo ni matunda ya jitihada zinazofanywa na Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) ambacho kiliratibu mazungumzo hayo
yaliyochukua zaidi ya saa mbili na nusu, katika Ikulu ya Kilimani,
wakati yale ya St. Gaspar yalichukua takriban saa moja na nusu.Viongozi
walioshiriki kikao hicho cha Ikulu ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania
Bara), Philip Mangula, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana,
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa na Mwanasheria wa chama hicho,
Tundu Lissu, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu
Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), Magdalena Sakaya.Wengine ni Mwenyekiti wa
NCCR Mageuzi, James Mbatia, Katibu Mkuu wake, Mosena Nyambabe,
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, Mwenyekiti wa UDP ambaye pia ndiye
mwenye zamu ya uenyekiti wa TCD, John Cheyo na Mwenyekiti wa UPDP pamoja
na mwakilishi wa vyama visivyokuwa na wabunge ndani ya TCD, Fahmi
Dovutwa.Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Rais Kikwete baada
ya kuanza kwa kikao hicho alitoa fursa kwa kila aliyekuwapo kuzungumza
na hapo zilijitokeza hoja mbalimbali, nyingi mwelekeo wake ukiwa ni
kutaka kusitishwa kwa Bunge Maalumu ili kutoa fursa kwa nchi kuendelea
na masuala mengine makubwa.Chanzo chetu kilisema:
Rais amekuwa msikivu kweli, amewasikiliza wote lakini ugumu ulianza kuonekana pale ilipotolewa kauli ya kuwauliza wale watu wa Ukawa kama wanaonaje wakirejea halafu hoja zao zikazungumzwa ndani ya Bunge Maalumu, yaani hawataki kabisa kusikia hilo.
Kuhusu hoja ya kusitishwa kwa Bunge,
habari zinasema ilijadiliwa kwa kirefu na wataalamu wa sheria wakijaribu
kutoa uzoefu wao, lakini kikwazo kilichoonekana ni Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba ambayo haimpi Rais mamlaka ya kusitisha Bunge.
Rais alisema hoja zao ni nzuri na zina mashiko, lakini suala kubwa likawa ni kwamba tunafikaje huko wanakopendekeza? Maana sheria iko kimya kuhusu mamlaka ya Rais kusitisha Bunge Maalumu, ndiyo maana sasa tulitoka Ikulu tukaenda St. Gaspar ili kujadili, ngoja tusubiri hiyo tarehe 8 maana siyo mbali
alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.Kauli ya TCDBaada
ya kikao cha St. Gasper, Mwenyekiti wa TCD, Cheyo aliwaambia waandishi
wa habari kwamba mazungumzo na Rais Kikwete yalikuwa mazuri na kwamba
wamekubaliana kukutana naye tena Septemba 8, mwaka huu baada ya kuwa
wamezifanyia kazi hoja ambazo zilijitokeza kwenye vikao hivyo.
Kama nilivyowaambia siku ile tulipokutana, tulikuwa na ajenda mbili tu kubwa, kwanza ni mchakato wa Katiba Mpya unavyokwenda na ajenda ya pili ni jinsi tunavyoweza kusonga mbele na kuwa na maandalizi ya uchaguzi mzuri mwakani
alisema Cheyo lakini akikataa kujibu maswali mengine ya
waandishi wa habari.Cheyo alisema baada ya kukutana na Rais Kikwete,
waliendelea na kikao cha viongozi wa vyama kwa ajili ya kuona jinsi ya
kuyafanyia kazi mambo yaliyojitokeza, hivyo wameamua kuunda kamati ndogo
ya watu wanne itakayoongozwa na Mbatia kwa ajili ya kutekeleza wajibu
huo.Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Kinana, Profesa Lipumba na Dk Slaa
ambao wamepewa wajibu wa kuwasilisha ripoti yao kwenye kikao cha
wenyeviti wa vyama vinavyounda TCD ili ijadiliwe kabla ya kikao cha
Septemba 8, ambacho hata hivyo, hakijafahamika kitafanyika wapi.Habari
zinasema miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa kazi ni pamoja na kuona kama
Bunge linaweza kusitishwa bila kuleta athari zozote za kisheria na
kisiasa, lakini wakizingatia uwapo wa makundi mengine ndani ya Bunge
hilo hasa wabunge wa kuteuliwa kupitia kundi la 201.
Lakini hapa kuna suala moja kwamba Ukawa wako nje ya Bunge, ni vigumu kuwaamrisha wale walioko ndani ya Bunge ili watekeleze matakwa yao, kwa hiyo kuna kazi kubwa sana ya kufanya
kilisema chanzo chetu.Mgomo wa UkawaDalili za
Ukawa kukataa kurejea bungeni zilianza kuonekana mapema baada ya
mazungumzo yasiyo rasmi ambayo yalifanyika katika moja ya kumbi za
Hoteli ya Dodoma ambako walikwenda kupata chai baada ya kuwasili.Wakati
wakitoka kwenye ukumbi huo kuelekea Ikulu Kilimani, baadhi yao
walisikika wakipeana tahadhari kwamba wasikubali wazo la kurejea
bungeni, ambalo ni dhahiri walikuwa wamepewa wakati wakinywa
chai.Baadaye ndani ya basi dogo wakati wakielekea Ikulu, Lissu alisikika
akisema:
Eti wanataka turejee, yaani tumekaa nje muda wote huo halafu leo hii tuje hapa kujadili kurudi, eti kurudi haiwezekani kabisa.
Pia
habari kutoka katika Ukumbi wa St. Gaspar zinasema hata katika kikao
hicho, viongozi hao walishauriwa kurejea bungeni ili hoja za kuahirishwa
kwa Bunge Maalumu zitolewe huko, lakini waligoma.Taarifa zinasema Ukawa
walijenga hoja kwamba Bunge Maalumu halipaswi kuendelea kwa sababu kuna
kila dalili kuwa muda uliopo hautoshi kukamilisha mchakato na
ikizingatiwa kwamba nchi inakabiliwa na mambo mengi ukiwamo Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Pia kulikuwa na hoja kuhusu mambo ya Daftari la Wapigakura na mabadiliko ya sheria ambazo zinagusa taasisi kama Tume ya Taifa ya Uchaguzi, sheria mbalimbali zinazihusu vyama vya siasa na mambo ya matokeo ya rais kuhojiwa nadhani
kilieleza chanzo kingine.Kushindwa
kupatikana kwa suluhu ya mchakato wa Katiba, kunaendelea kuuweka
mchakato huo njiapanda hasa ikizingatiwa kwamba Bunge Maalumu
linaendelea kesho kupokea ripoti za kamati kuhusu uchambuzi wa sura 15
za Rasimu ya Katiba.




0 comments:
Chapisha Maoni