Alhamisi, Septemba 04, 2014

MAWAZIRI MBEYA KATIKA BIFU!!!

Kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 minyukano ilitawala katika siasa za Jimbo la Kyela, sasa ni zamu ya Jimbo la Ileje ambako minyukano imeanza huku manaibu waziri wawili wakitajwa.
Katikati ya mgogoro huo wapo viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ileje na Mkoa wa Mbeya, mtihani sasa upo CCM Taifa kutengua mtego huo, vinginevyo unaelekea kukidhalilisha chama hicho kwa mara nyingine Mkoani hapa.
Mawaziri wanaotajwa katika mgogoro huo ni Naibu Waziri wa Viwanda, Janet Mbene na Naibu Waziri wa Kilimo, Godfrey Zambi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.
Zambi anaingia kwenye mgogoro huo kutokana na nafasi yake kama Mwenyekiti wa CCM Mkoa, ambaye anadaiwa alisimamia maamuzi ya kuisimamisha Kamati ya Siasa ya chama hicho Wilaya ya Ileje kwa madai ya kukidhalilisha chama wilayani humo.
Waziri Mbene ameingizwa kwenye mgogoro huo baada ya Kamati ya Siasa ya Mkoa kumtaka ajieleze uhusika wake kwenye mgogoro huo, pamoja na ukweli kwamba yeye si mjumbe wa Kamati hiyo ya Siasa Wilaya ya Ileje, iliyosimamishwa.
Hatua ya Kamati ya Siasa ya Mkoa inayomtaka Naibu Waziri huyo kujieleza, imeibua mjadala zaidi, huku wengi wakiamini kuwa ni njama za kumbana mama huyo asiweze kuwania jimbo kati ya Ileje na Mbeya Mjini ambako imevuma kuwa huenda akagombea.
Katika mahojiano yake na Raia Mwema, kuhusu madai ya yeye kuwania Jimbo la Ileje, Mbene anasema:
Kosa langu kuwa mtoto wa Ileje, mimi kule ni nyumbani, wazazi wangu wanapohitaji nisaidie, ninasaidia, mimi ni mtoto wao, wanayo haki kuwatumia watoto wao, haya mambo ya ubunge nayasikia yanazungumzwa tu, wao ndio wanayajua, nachojua mimi nasaidia wazazi wangu, ndugu zangu.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Mbeya, Bashiru Madodi, Kamati ya Siasa ya Mkoa huo, ikiwa imekasimiwa madaraka na Halmashauri ya Mkoa, CCM, imeisimamisha Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Ileje kwa kosa la kufunga ofisi ya chama ya Wilaya hiyo kwa siku kumi.
Ni uhaini kuzuia shughuli za chama, wamekifanya chama kunuka mbele ya jamii
alisema Madodi katika mahojiano maalumu

0 comments:

Chapisha Maoni