Kwenye maisha yetu ya kila siku tunakutana na watu mbalimbali ambao wametoka katika mazingira mbalimbali. Watu hawa tunaweza kukutana nao kwenye masomo, kwenye kazi na biashara, na hata kwenye mikusanyiko mbalimbali ya maisha.
Watu tunaokutana nao kwenye maisha wana athari kubwa sana kwenye maisha yetu(soma; wanaokuzunguka wanamchango mkubwa kwenye maisha yako). Kuna ambao wana athari chanya na kuna wenye athari hasi kwenye maisha yetu.
Leo tutaangalia watu wenye athari hasi kwenye maisha yetu na jinsi tunavyoweza kujikinga na athari hizo. Kutowajua watu hawa na kutotambua athari zao kwenye maisha yetu kumepelekea wengi wetu kuyumbishwa na watu hawa.
Watu hawa wanaweza kuwa ni watu wa karibu sana kwetu kama ndugu na jamaa, wenza(mke/mume), wasimamizi wa kazi, au hata waalimu. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuwatambua na kuweza kuepukana na athari zao.
Kutokana na mazingira mbalimbali tuliyokulia na kutokana na changamoto mbalimbali tulizopitia kwenye maisha kuna makundi mbalimbali ya watu ambao wana athari hasi kwa wenzao. Hapa tutazungumzia makundi matatu ya watu hawa.
1. WATU WENYE MTIZAMO HASI JUU YA MAISHA YAO NA MAISHA YA WENGINE
Kwenye maisha yako umeshakutana na watu wengi wa aina hii. Wao kwenye kila utakachosema ama utakachofanya watatafuta njia ya kukukosoa. Ni watu ambao wana mtizamo hasi na kwenye kila kitu huwa wanatafuta makosa. Kwa kutowajua watu hawa unaweza kujikuta kila siku unakata tamaa kwenye mambo unayoyafanya. Na mbaya zaidi inapotokea mtu wa aina hii akawa ni bosi wako kazi inaweza kuwa ngumu sana.
2. WATU WASIOJIAMINI NA WASIOAMINI KAMA WENZAO WANAWEZA
Kuna watu ambao hawajiamini na pia hawaamini kama wenzao wanaweza kufanya mambo makubwa kwenye maisha yao. Watu hawa ni wakatishaji tamaa wakubwa na kama umezungukwa nao na hujawatambua ni vigumu sana kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako. Kila utakapojaribu kufanya jambo la tofauti watu hawa watakupa sababu lukuki kwa nini utashindwa. Na kama watu hawa ni watu unaowaheshimu kwenye maisha kama wazazi au ndugu wa karibu unajikuta unafata ushauri wao na kutofanya lolote.
3. WATU AMBAO MAISHA YAMEWAUMIZA SANA NA FARAJA PEKEE WANAYOIPATA NI WAO KUWAUMIZA WENGINE
Watu hawa ni wengi sana kwenye jamii, ni watu ambao maisha yamewaumiza vya kutosha na hawana chochote cha kuwafurahisha na hivyo furaha pekee wanayoipata nikuona wengine wanaumia kama wao. Watu hawa wanaweza kuwa wasimamizi wako kwenye kazi au masomo au watu wanaotakiwa kutoa huduma fulani. Kutowajua watu hawa unaweza kuwa unaumia sana, ila ukiwajua utaelewa kwamba wao ndio wanaumia zaidi.
Makundi haya ya watu yanachangia kuwarudisha watu wengi nyuma. Na kwakuwa jamii imejaa watu wengi wa aina hii ndio sababu kubwa ya watu wengi kwenye jamii kutoendelea.
Chunguza maisha yako na wanaokuzunguka na kisha angalia malengo na mipango ya maisha yako. Angalia ni watu gani waliowahi kukurudisha nyuma ama kukuumiza kwa njia yoyote ile. Baada ya kuwajua watu hawa epuka athari zao na endelea na maisha yako.
Naposema epuka athari zao simaanishi uwatenge watu hawa. Wanaweza kuwa ni watu muhimu kwako kama ndugu, mke/mume, bosi au hata mwalimu. Njia pekee ya kuepuka athari zao ni kutotilia maanani maneno yao au matendo yao.
Kama mtu anakupa sababu kwa nini utashindwa unaweza kumsikiliza kisha ukampuuza bila hata ya kumuonesha kwa sababu umeshamjua. Kama mtu anafanya jambo la kukuumiza furahia na endelea na maisha yako kwa kuwa yeye ndio anaumia zaidi. Kama mtu anatafuta makosa kwenye kitu unachofanya ama unachosema mpuuzie na endelea na mambo yako.
Usitumie muda wako mwingi kupingana ama kubishana na watu wa aina hii. Kwa kufanya hivyo utajikuta unapoteza nguvu nyingi na mwisho wa siku wewe ndio utaumia, maana wao wanafurahia wanachofanya.
0 comments:
Chapisha Maoni