Majonzi ya wenyeji wa Kombe la Dunia, Brazil yalizidi baada ya
Uholanzi kuwacharaza 3-0 kwenye mechi ya kuamua nafasi ya tatu jijini
Brasilia Jumamosi usiku.
Huku wakiendelea kuomboleza kuchabangwa 7-1 na Ujerumani katika nusu
fainali, Brazil walijipata mashakani zaidi dakika tatu pekee baada ya
kipenga cha mwanzo wakati Robin van Persie alipopachika wavuni penalti
na hivyo kuwapa Uholanzi uongozi. Daley Blind alifaidika kutoka kosa la
beki David Luiz dakika zilipokatika 17 kuongezea chumvi kwenye kidonda
cha wenyeji ambao walikuwa na nyota wao maarufu aliyejeruhiwa, Neymar,
akitizama kutoka benchi. Georginio Wijnaldum alikamilisha fedheha ya
Wabrazil katika muda wa ziada kwa bao la tatu na hivyo kuzidisha gadhabu
kutoka mashabiki ambao walichukizwa na kusambaratika kwa mabingwa hao
wa mara tano wa Kombe la Dunia. Brazil walipoteza mechi mbili mtawalia
nyumbani kwa mara ya kwanza tangu 1940 na walimaliza shindano hili
wakiwa wamepokea mabao 14 ambayo ni mengi zaidi kwa timu zinazoshiriki
Kombe la Dunia tangu 1986. Uholanzi wameuchukua nafasi ya tatu na
kumaliza shindano hili bila kuonja kichapo baada ya kuondolewa semi
fainali kupitia mikwaju ya penalti. Walipoteza kiungo wao tegemeo,
Wesley Sneijder, ambaye alilazimishwa kukosa mechi hiyo baada ya kupata
jeraha dakika chache kabla ya mechi hiyo kuanza huku Jonathan de Guzman
akidhibiti nafasi yake.
0 comments:
Chapisha Maoni