Mkataba wa Gesi umevuja: Tanzania kupoteza shs 1.6 trilioni kwa mwaka
-Norway kujirudishia misaada yake yote nchini kupitia mkataba huu
Zitto Kabwe, Mb
Mkataba wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji wa Gesi Asilia
(PSA) kati ya Shirika la Mafuta Tanzania na Kampuni ya Mafuta ya Norway
umevujishwa (https://onedrive.live.com/view.aspx?cid=0EC42B180C06D0B8&resid=EC42B180C06D0B8%21107&app=WordPdf).Toka
Mkataba huo uvuje na kuanza mijadala kwenye mitandao ya kijamii, habari
zake zimekuwa zinazimwa na hivyo kukosa kabisa mjadala mpana kitaifa na
hasa kwa wananchi wenye rasilimali zao. Mwanzoni wengi wetu tulidhani
(kwa makosa) kuwa tatizo la mkataba huu ni eneo la umiliki wa kampuni tu
(shareholding) kulingana na namna ulivyowasilishwa, kumbe mgawanyo
mzima wa mapato unakwenda kinyume na maelezo ya Serikali na TPDC kwa
umma.
Mkataba uliovuja unaonyesha kwamba makubaliano ambayo
Serikali imeingia na Wawekezaji hawa kutoka Norway yanaenda kinyume
kabisa na mfano wa mkataba unaotakiwa kusainiwa (Model PSA). Kwa mujibu
wa makala iliyoandikwa na jarida la mtandaoni ( http://africanarguments.org/2014/07/04/leaked-agreement-shows-tanzania-may-not-get-a-good-deal-for-gas-by-ben-taylor/
) Tanzania itapoteza zaidi ya shilingi 1.6 trilioni kila mwaka
kulingana na viwango vya uzalishaji wa gesi asilia katika Kitalu namba
2. Kitalu hiki kinamilikiwa na Kampuni ya StatOil ya Norway na kampuni
ya ExxonMobil ya Marekani. Norway ni nchi inayosifika duniani kwa
kupambana na rushwa na kwa kutumia vizuri rasilimali yake ya mafuta.
Uchambuzi nilioufanya kulingana na viwango vya mgawo wa mapato kati ya
‘model’ PSA na mkataba huu unaonyesha kwamba Tanzania itapata mgawo
kiduchu sana na kinyume na mgawo unavyopaswa kuwa. Mgawanyo ni kama
ifuatavyo katika majedwali hapa chini; Ikumbukwe kuwa mgawanyo huu
hupatikana baada ya mwekezaji kuondoa gharama zake za uzalishaji,
kinachobakia ndio hugawanywa kati ya mwekezaji na Tanzania.
Jedwali 1 Mkataba wa mgawanyo wa Mapato unaopaswa kutumiwa na TPDC (Model PSA) katika Mikataba na Wawekezaji
Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day) Mgawo wa TPDC (Profit Gas)
Mgawo wa Mwekezaji (Profit Gas)
0 249.999 50 50
250 499.999 55 45
500 749.999 60 40
750 999.999 65 35
1000 1249.999 70 30
1250 1499.999 75 25
1500 Above 1500 80 20
Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day) Mgawo wa TPDC (Profit Gas)
Mgawo wa Mwekezaji (Profit Gas)
0 249.999 50 50
250 499.999 55 45
500 749.999 60 40
750 999.999 65 35
1000 1249.999 70 30
1250 1499.999 75 25
1500 Above 1500 80 20
Jedwali 2 Mkataba wa mgawanyo wa Mapato kati ya TPDC na Statoil/ExxonMobil.
Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day) Mgawo wa TPDC (Profit Gas)
Mgawo wa Mwekezaji (Share of Profit Gas)
0 299.999 30 70
300 599.999 35 65
600 899.999 37.5 62.5
900 119.999 40 60
1200 1499.999 45 55
1500 Above 1500 50 50
Viwango vya uzalishaji kila siku (MMscf per Day) Mgawo wa TPDC (Profit Gas)
Mgawo wa Mwekezaji (Share of Profit Gas)
0 299.999 30 70
300 599.999 35 65
600 899.999 37.5 62.5
900 119.999 40 60
1200 1499.999 45 55
1500 Above 1500 50 50
Ukilinganisha majdwali haya utaona kwamba mgawanyo wa mapato
utafaidisha zaidi kampuni ya StatOil na ni kinyume kabisa na mkataba
unavyopaswa kuwa.
Wakati mgawo wa nusu kwa nusu upo katika
uzalishaji wa chini kabisa kwenye ‘model PSA’, kwenye mkataba wa StatOil
mgawo huo upo kwenye uzalishaji wa juu kabisa. Ukilinganisha mgawanyo
huu wa mapato, iwapo kiwango cha ‘model PSA’ kingetumika Tanzania
ingepata shilingi 1.6 trilioni zaidi ya kiwango itakachopata kwenye
mkataba wa sasa uliovujishwa. Hii ni kutokana na Bei ambazo Shirika la
Fedha la Kimataifa limeweka katika uchambuzi wake (https://www.imf.org/external/pubs/ft/scr/2014/cr14121.pdf ) kuhusu Gesi asilia ya Tanzania.
Kwa mujibu wa Mwandishi Ben Taylor katika makala iliyotajwa hapo juu,
kiwango cha mapato ambacho Kampuni ya StatOil ya Norway itajipatia
kutokana na mkataba huu wa kinyonyaji, katika kipindi cha miaka 15 ya
kuzalisha Gesi Asilia nchini itakuwa ni sawa sawa na misaada yote ambayo
Tanzania imepata kutoka Norway toka Tanzania ipate uhuru wake mwaka
1961. Tangu Tanzania ipate Uhuru Norway imetoa misaada ya thamani ya
$2.5 bilioni, wakati kwa mkataba huu na Kampuni ya StatOil ambayo
inamilikiwa na Serikali ya Norway, kwa miaka 15 watapata $5.6 bilioni.
Kwa hiyo kwa miaka 7 tu Norway itakuwa imerudisha misaada yote yake mara
mbili zaidi!
Kuvuja kwa Mkataba huu kumesaidia sana kuona ukweli
wa matamko ya viongozi wetu kuhusu ni namna gani Tanzania itafaidika na
utajiri wake wa gesi. Kama kwa mkataba huu mmoja tu Taifa litapoteza
matrilioni ya fedha kiasi hiki, ipoje hiyo mikataba mingine 29? Hivi
sasa ugunduzi wa Gesi Asilia nchini ni lita za ujazo trilioni 51 ambayo
ni sawa na mapipa bilioni 10 ya Mafuta. Katika Gesi Asilia yote
iliyopatikana nchini, StatOil peke yao wana jumla ya lita za uzajo
trilioni 20, sawa sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4 (zaidi ya mafuta
yaliyogunduliwa nchini Uganda na Ghana kwa pamoja). Hata hivyo utajiri
wote huu utainufaisha zaidi Norway na Marekani kupitia makampuni yao
kuliko watu wa Tanzania. Watanzania watabakia wanapewa misaada ya
vyandarua na mataifa haya ilhali wanafaidi Gesi Asilia yetu.
Natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini kutoa tamko kuhusu mkataba
huu kati ya Shirika la TPDC na StatOil. Vile vile Kampuni hii ya StatOil
kutoka nchi rafiki mkubwa wa Tanzania ina wajibu wa kutoa maelezo ya
kina kuhusiana na mkataba huu. Serikali ieleze ni hatua gani inachukua
kurekebisha Mkataba huu. StatOil nao waeleze watachukua hatua gani
kuhakikisha wanaacha unyonyaji huu mkubwa na wa aibu kwa Taifa la
Norway.
Sasa ni wakati mwafaka Watanzania kuweza kuona mikataba
yote ya Gesi na Mafuta ambayo Serikali imeingia na Wawekezaji. Uwazi wa
Mikataba sasa. Nimewahi kuandika huko nyuma (http://zittokabwe.wordpress.com/2012/09/17/press-release-contracts-review-is-a-publicity-stunt-and-creation-of-unnecessary-uncertainty-in-the-sector/
) kwamba njia pekee ya Watanzania kufaidika na utajiri wa rasilimali
zao ni kuhimiza uwazi wa Mikataba. Mkataba huu wa StatOil uliovujishwa
uwe ni chachu ya kulazimisha Serikali na Makampuni kuweka mikataba yao
wazi. Tuanze mashinikizo haya sasa kwa faida ya vizazi vijavyo.
0 comments:
Chapisha Maoni