Mkurugenzi wa Kampuni ya Benchmark Productions inayoendesha shindano la
kusaka vipaji vya muziki, Bongo Star Search (BSS), Rita Paulsen ‘Madam’
amesimulia mateso aliyopitia takriban mwaka sasa (siku 365) baada
kuvunjika mguu mwaka jana alipopata ajali ya gari katikati ya Jiji la
Dar.
Madam Rita alisema kwa kusikitisha kwamba, baada ya kupata ajali
alitibiwa kwenye Hospitali ya Muhimbili lakini madaktari walimwambia
aliteguka tu kumbe alikuwa amevunjika mfupa.
Nimepitia mateso makubwa. Mwaka jana baada ya kupata ajali na kuvunjika mguu nilipopelekwa Muhimbili waliniambia nimeteguka tu, na wakaamua kunifunga hogo ambalo baadaye walinifungua na kuniambia nimepona
alisimulia Madam Rita na kuongeza:
Baada ya pale nilianza kujiachia hata niliposikia maumivu na kuwaambia walisema niukanyagie tu kwamba hali hiyo ingebadilika kwa sababu ulielekea kupona, kumbe nilikuwa nimevunjika kabisa mfupa na kama ningejua siku nyingi hata nisingejiumiza kiasi hicho.
Ujue baada ya kuambiwa hivyo, nilishangaa kuona maumivu yanazidi, nikaamua kwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuuangalia zaidi mguu wangu kwa sababu maumivu yalikuwa yakiongezeka kila siku.
Nilikwenda kwenye Hospitali ya Morning Site ya Afrika Kusini ambapo nilifanyiwa upasuaji na kugundulika nilivunjika mfupa na kwamba tayari nilipokuwa nikitembea ilikuwa ikipandiana.
Ona sasa nilivyoteswa na mguu huu maana ajali nilipata mwaka jana na huu upasuaji nimefanyiwa mwaka huu Afrika Kusini.
Kiukweli hospitali zetu saa nyingine zinatusababishia shida ambazo siyo za lazima maana kama awali wangenifanyia upasuaji wakati nawaambia ninaumia baada ya kunitoa hogo, basi leo ningekuwa nafanya shughuli zangu.
Naona bora pale Fame Centre (Dar) maana wao waligundua tatizo na kunishauri kwenda Sauzi ambapo nimefanyiwa upasuaji na mguu unaelekea kupona kwa sababu mwanzo nilikuwa natumia magongo mawili lakini ona leo ninajikongoja kwa gongo moja ambalo nalo si muhimu sana sasa.
0 comments:
Chapisha Maoni