Ijumaa, Julai 18, 2014

CCM MBEYA YATAPELIWA

Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mbeya kimeingia katika mgogoro na wapangaji wake, ambao hawataki kulipa madeni ya pango kwa madai mali zinazomilikiwa na chama hicho si zao bali wamezipora.
Kutokana na hali hiyo, inaelezwa chama hicho kimeamua kuingia mkataba na Kampuni ya Yono Auction Mart wa kukusanya mapato kwa nguvu.
Uchunguzi uliofanywa na FICHUO, umebaini baadhi ya wakazi wa jijini hapa wanaofanya biashara na wanaoishi kwenye viwanja vya Sabasaba na kumbukumbu ya Sokoine, hawataki kukilipa chama hicho zaidi ya sh milioni 40, kwa madai kuwa mali wanazomiliki si halali na zimetokana na jasho la wananchi waliojitolea kwa hali na mali kuzijenga.
Baadhi ya wananchi waliopanga na kupinga utozwaji wa kodi (majina tunayo), walidai kuwa hawapo tayari kuilipa CCM na wanachotaka, kuona mali hizo zinarudishwa mikononi mwa serikali ili zitumiwe na wananchi wote, kwa kuwa si mali ya chama chochote cha siasa na zilipatikana kutoka kwenye michango ya wananchi wote bila kujali itikadi ya vyama.
Hali hiyo imesababisha uhasama wa chini kwa chini uzidi kufukuta kati ya wananchi wa Jiji la Mbeya na CCM, baada ya chama hicho kuingia mkataba na Yono waliopewa jukumu la kukusanya madeni.

0 comments:

Chapisha Maoni