FAMILIA mbili mjini Mpanda zimejikuta zikiingia katika uhasama mkubwa,
kiasi cha kupigana fimbo na ngumi makaburini katika ugomvi wa kugombea
kuzika mwili wa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.
Sababu kubwa ya mpasuko huo imeelezwa kuwa ni mahari, kwani wazazi
upande wa mama wa mtoto huyo walikuja juu na kumzuia baba wa mtoto,
Joseph Bacho mkazi wa Mtaa wa Kawajense- Madukani mjini Mpanda asishiriki
katika shughuli zozote za maziko ya mtoto wake wakidai hawamtambui kwa
kuwa hajatoa mahari kwa binti yao.
Inaelezwa kuwa, Joseph na mzazi mwenzake, Anna Kizo ambaye pia ni
mkazi wa Mtaa wa Kawajense –Madukani walimzaa mtoto Junior Bacho nje ya
ndoa ambapo hadi umauti unamfika mtoto huyo, baba yake mzazi alikuwa
hajajitambulisha kwa upande wa mwanamke wala kutoa mahari.
Na kwamba, tangu kuzaliwa kwa mtoto huyo, alikuwa akiishi na kulelewa
na mama yake mzazi, Anna nyumbani kwa wazazi wake katika Mtaa wa
Kawajense.
Kwa mujibu wa waombolezaji ambao hata hivyo hawakuwa tayari kutajwa
majina gazetini, vurugu hizo ziliibuka baada ya upande wa ndugu wa baba
wa mtoto kuweka msiba nyumbani kwao na kuandaa taratibu za kumzika mtoto
huyo.
Hata hivyo, kitendo hicho kilipingwa na upande wa mama wa mtoto,
ukisema ndio wenye haki ya kumzika mtoto huyo ambaye hawakuwahi
kumtambua kisheria baba yake mzazi.
Ndugu wa upande wa baba ulifanikiwa kuchimba kaburi, kuutoa mwili
mochari na kuufikisha nyumbani tayari kwa maziko, lakini vurugu za
upande wa pili ikiwa pamoja na ndugu upande wa mama kufukia kaburi,
zilisimamisha shughuli zote, huku malumbano yakishika hatamu hadi askari
wa jeshi la polisi kupitia kikosi chake cha kuzuia fujo (FFU)
kilipolazimika kuingilia kati na kusimamia shughuli za kuurudisha mwili
katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda.
Inaelezwa kitendo cha upande wa mama wa mtoto kufukia kaburi ndiko kulikochangia kuchochea vurugu hadi FFU walipoingia kati.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi , Dhahiri Kidavashari
amethibitisha kutokea kwa mkasa huo kwamba hakuna mtu yeyote
aliyejeruhiwa katika vuta nikuvute hiyo pia hakuna ayekamatwa kuhusiana
na tukio hilo ambalo ni la kijamii zaidi.
0 comments:
Chapisha Maoni