Wakati wafuasi wa dini tukufu ya Kiislamu duniani kote wameshaanza
kuufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, Bacary Sagna beki wa timu ya taifa
ya Ufaransa ameeleza kinagaubaga kwamba, ataendelea kufunga saumu ya
mwezi huo, licha ya kukabiliwa na kibarua kigumu cha mashindano ya kombe
la dunia ambayo yameingia hatua ya pili ya mtoano. Sagna amesisistiza
kwamba, ataendelea kufunga saumu ya mwezi mtukufu, licha ya kukabiliwa
na mechi ngumu kwenye michuano hiyo. Sagna ameviambia vyombo vya habari
vya Ufaransa na hapa tunamnukuu: 'Mimi nataka kufunga saumu nchini
Brazil, kwa kuwa ni Muislamu. Dini tukufu ya Kiislamu inanipa fursa ya
kutofunga saumu nikiwa katika mazingira maalumu kama vile safari na
maradhi, lakini pamoja na kukabiliwa na mashindano ya kombe la dunia
nchini Brazil sitaki kufungulia. Nitaendelea kufunga saumu ya mwezi
mzima wa Ramadhani, Inshaallah', mwisho wa kunukuu. Licha ya Bacary
Sagna wachezaji wengine wengi wanaoozichezea timu za taifa za Ufaransa,
Algeria, Nigeria na Ujerumani wameendelea kusisitiza kwamba watafunga
saumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani licha ya kukabiliwa na mechi ngumu
za kombe la dunia. Hapo kesho, Nigeria 'Tai wa Kijani' itapimana misuli
na Ufaransa, huku timu ya taifa ya Algeria 'Mbweha wa Jangwani'
itajitupa uwanjani siku ya Jumanne kupambana na Ujerumani katika hatua
ya 16 bora. Inafaa kuashiria hapa kuwa, hivi karibuni Jiri Dvorak
mjumbe mwandamizi wa Kamati ya Afya ya Shirikisho la Soka Duniani FIFA
alisema kuwa, wachezaji Waislamu watakaofunga mwezi mtukufu wa
Ramadhani, hawataathirika kiafya wakati wa kuendelea michuano hiyo
nchini Brazil.
0 comments:
Chapisha Maoni