Macho ya wakazi wa Segerea jijini Dar es Salaam yanatufuata kila
tunakokatiza mimi na Chuche Atukuzwe Pemba, hata baadhi walisimama ili
wayaridhishe macho yao kwa kile wanachokiona.
Baada ya kututazama kwa mshangao, baadhi
wanaonekana kunong’onezana jambo, lakini wapo pia ambao hawatushangai,
bali wanamsalimia Chuche kwa heshima.
Unajua kwa nini macho ya watu hawa yanatutazama kwa mshangao?
Ni kwa sababu Chuche, mwanaume wa miaka 45, ambaye aliwahi kuoa na sasa ana watoto wawili kuvaa mavazi ya kike.
Siyo hivyo tu, Chuche pia amejipaka wanja, rangi
ya mdomo na kuvaa hereni na shanga za miguuni, huku kucha zake za mikono
na miguu nazo zikiwa zimepakwa rangi na chini, akiwa amevalia viatu vya
kike.
Hali hii ya Chuche, haiwashangazi wanajamii wengi
kama mimi na wewe pekee, bali hata wanafamilia wenzake, akiwamo mama
na ndugu zake.
Hakuna anayefahamu nini kilimpata Chuche, msomi
mwenye Shahada ya Biashara na Diploma ya Usanifu wa Majengo kutoka
Urusi, ambaye ni mwerevu katika masomo, ambaye awali alikuwa tegemeo la
familia na pengine kama siyo mabadiliko haya, basi angekuwa hazina
muhimu kwa taifa.
Nafika nyumbani kwa Chuche, naye ananikaribisha
hadi katika chumba chake cha kulala. Humu nakutana na mandhari kama yale
ya chumba cha mtoto wa kike.
Ana kabati la viatu lililopangwa viatu vya kike,
pia kuna meza ya vipodozi iliyojaa hereni, bangili, mikufu, manukato na
mafuta ya aina mbalimbali. Siku niliyokutana naye, alikuwa amevaa
blauzi nyeupe ya mikono mifupi na kibana msuli (skin tight).
Ninapomuuliza kwa nini amegeuka na kuwa na tabia za kike? Chuche
ananijibu kwa kifupi:
Ni hobi yangu.
Chuche anasema kuwa anapenda kuvaa mavazi ya kike kwa sababu ni kitu anachokipenda na wala siyo kwa sababu nyingine yoyote.
Je, Chuche ni shoga?
Mimi siyo shoga, mimi ni mwanaume rijali, ushahidi ni watoto wangu hao. Lakini napenda kuvaa mavazi ya kike tangu nikiwa mdogoanasema. Chuche alizaliwa mwaka 1969 jijini Dar es Salaam akiwa ni mmoja wa watoto wa familia ya marehemu Curthbet Pemba.
Watu wananiandama, wananipeleka hospitali eti wanasema nina kichaa, lakini mimi ni mzima, isipokuwa napenda kuvaa mavazi ya kike. Sidhani kama kuvaa hivi naingilia maisha ya mtu au namkera mtu, ni hobi yanguanasema.
Chuche anasimulia kuwa baada ya kumaliza kidato
cha nne katika Sekondari ya Jitegemee, Mgulani, alipata ufadhili wa
masomo kwenda nchini Urusi.
Nilipata division one na nilikuwa mwanafunzi bora, kama unabisha nenda kaulize Jitegemee. Kwa sababu nilifaulu vizuri hasa masomo ya hesabu na sayansi, nilipata nafasi ya kusoma Urusianasema Chuche.
Anaeleza kuwa alipofika Urusi, alianza kusoma
Stashahada ya Usanifu wa Majengo (architecture) kwa miaka miwili, kabla
ya kuendelea na masomo ya Shahada ya Biashara katika Chuo cha Haipei
Polytechnic.
Anasema kwamba muda mfupi baada ya kumaliza
masomo, alifanya kosa nchini humo na alifungwa jela. Hata hivyo, hakukaa
sana kabla ya kuachiwa huru.
Kule kukaa jela kulisababisha nikaacha vyeti vyangu vyote na nikarudi nchini kwa harakaanasema bila kuweka wazi kosa alilolifanya. Akiwa nchini Urusi, Chuche alipata mwenza, aliyejulikana kama Okhsana na wakati akirejea nchini, alirudi naye na kuanza maisha kama mume na mke.
Wakiwa nchini, Chuche na Okhsana, walibahatika
kupata watoto wawili, wa kike na wa kiume. Kwa bahati mbaya, Okhsana
alifariki dunia, mwaka 2002 kwa ugonjwa wa saratani na kumwacha Chuche
na watoto hao.
Mama yake Chuche
Mama yake Chuche, Matilda Pemba anasema kuwa
kinachomsumbua Chuche bado ni kitendawili, kwani wameshahangaika sehemu
tofauti ili kumwondoa katika hali hiyo ya kuvaa mavazi ya kike bila
mafanikio.
Kama mama niliyezaa mtoto wa kiume, nikajua ni wa kiume silifurahii jambo hili hata kidogo. Nimehangaika sana kujua tatizo ni nini, lakini bado sijaona mafanikioanasema. Anabainisha kwamba, Chuche alianza kubadili tabia mara tu baada ya kurudi kutoka Urusi.
Aliporudi hapa alikuwa na mabadiliko, tulishangaa hata vyeti vyake hakurudi navyo. Ingawa alirudi na mke kabisaanasema Matilda.
Anasema iliwashangaza wanafamilia kumwona akivaa
mavazi ya kike, wakati mwingine sketi na blauzi, wakati mwingine ‘skin
tight’ na blauzi, hata khanga.
Nilidhani ni dawa za kulevya, lakini tulipompima damu haikuonekana kuwa na dawa za kulevya. Nilifikiri labda ameanza mapenzi ya jinsia moja, lakini hilo pia siyo kwani angekuwa hivyo kila mtu angefahamu hata mimi ningejuaanasema mama Chuche.
Anaeleza kuwa wamejaribu kumtibu Chuche kwa
madaktari wa magonjwa wa akili hata kufika Mirembe, lakini bado hakuna
nafuu yeyote, wala dalili ya kurudi katika hali yake ya kawaida.
Tumempeleka kwenye maombi ya dini zote, Waislamu kwa Wakristo, lakini Chuche hakupata nafuu. Wanatuambia ana pepo la kike,anasema
Matilda anasema kwamba ili kumzuia kuvaa mavazi ya
kike, wakati mwingine huzichoma nguo hizo, lakini baada ya muda, Chuche
hununua nyingine.
Rafiki wa Chuche
Mmoja wa marafiki wa Chuche, Hans Kitomanga
anasema kuwa anamfahamu Chuche kwa muda mrefu, ingawa bado hafahamu
historia ya Chuche kuvaa mavazi ya kike.
Tangu nimekutana naye, namwona akivaa mavazi haya, nilimshangaa awali, lakini baadaye nikagundua kuwa ni mtu wa kawaida tu, tena ana akili zisizo za kawaida
anasema Kitomanga.
Anabainisha kuwa maisha ya Chuche yanawashangaza
wengi na kuleta hisia nyingi, lakini kwake anamchukulia kama rafiki wa
karibu anayehitaji bega la kuegemea.
Siyo hivyo tu, Kitomanga pia anakataa katakata
hisia kuwa huenda Chuche anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja na
kusema:
Watu hao wanajulikana hata kwa kuwaangalia tu na siyo lazima wavae mavazi ya kike kama anavyofanya Chuche.
Nini tatizo la Chuche?
Profesa Sylvia Kaaya wa Kitengo cha Magonjwa ya
Akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH) anasema kuwa watu
kama Chuche kwa kitaalamu wanaitwa ‘Transvestite’ au wanaopenda kuvaa
mavazi ya jinsi tofauti (cross dressing).
Watu hawa kwa kwaida hujisikia furaha na amani wanapovaa mavazi ya jinsi tofauti, wakati mwingine kuwa na tabia za jinsi hiyo.
Baadhi ya wanawake huvaa kama wanaume, lakini asilimia kubwa wanaopenda kuvaa mavazi ya jinsi tofauti ni wanaume.
Tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani zimethibitisha kuwa
wanaopenda kuvaa mavazi ya jinsi tofauti hawafanyi mapenzi ya jinsia
moja. Profesa Kaaya anasema kuwa wanaume wengi wanaopenda kuvaa mavazi
ya kike, bado wanapenda kuwa wanaume na hawana mshawasha wa kuwa
wanawake kwa kuwekewa vichocheo vya kike.
Kinyume na hapo, wanaume ambao hawapendi kuwa
wanaume na wanajisikia kuwa siyo wanaume ndani ya mioyo yao kwa
kitaalamu huitwa, ‘gender dysphoria’ au kutoridhika na jinsi uliyozaliwa
nayo.
Hali ya kutoridhika na jinsia zao inapowasababishia kuchukua hatua ya kubadili jinsi hizo, huitwa ‘transsexuals’
0 comments:
Chapisha Maoni