Jumamosi, Mei 03, 2014

RAIA WA URUSI ANAYEIZUNGUKA DUNIA KWA MIGUU TAYARI AMEFIKA TANZANIA

Raia wa Urusi, Sergey Chikachev anayezunguka mataifa mbalimbali duniani kwa miguu,  juzi amewasili nchini akitokea Kenya na anatazamiwa kuzunguka mikoa mbalimbali kwa siku 30.
Akizungumza mjini Moshi jana, Chikachev ambaye ameshazunguka mataifa 80, alisema akiwa nchini, atakwenda vijijini kujifunza utamaduni na maisha ya makabila mbalimbali.
Kwa siku chache tangu niwasili hapa (Moshi) nimebaini Watanzania ni watu wenye hazina kubwa ya ukaribu… naamini nitajifunza mengi yatakayonisaidia kuandika kitabu changu
alisema.
Chikachev alisema atakitumia kitabu chake hicho, kupeleka ujumbe wa amani kwa mataifa hayo na kuhamasisha urafiki kati ya makabila ya mataifa mbalimbali atakayoyatembelea duniani.
Kwa mujibu wa Chikachev, alianza kutembelea mataifa hayo kwa miguu tangu mwaka 2004 na ameshazunguka Ulaya, Asia, Australia, Marekani na sasa bara la Afrika ambapo kwa sasa yupo nchini Tanzania.
Chikachev alisema baada ya kumaliza safari yake nchini, anatarajia kwenda Uganda, Rwanda, Burundi, Namibia, Botswana, Congo, Nigeria na baadaye Cameroon na atahitimisha ziara zake hizo mwaka 2017.
Hata hivyo alisema safari yake hiyo imekuwa ikikutana na changamoto nyingi na wakati mwingine amekuwa akipata lifti kutoka kwa madereva wa malori lakini hilo limekuwa likitokea mara chache.
Raia huyo wa Urusi alisema kwa baadhi ya mataifa, amekuwa akipatiwa ufadhili wa usafiri wa ndege au majini katika maeneo ambayo hawezi kutembea kwa miguu kutoka taifa moja kwenda lingine.

0 comments:

Chapisha Maoni