Ugomvi wa mara kwa mara baina ya wapenzi, marafiki
ama hata jamii unaongeza hatari ya kufa kwa watu wenye umri wa
makamo.Haya ni kwa mujibu wa watafiti nchini Denmark.
Watafiti wamesema kuwa wanaume na wale ambao hawana kazi wako katika hatari Zaidi.
Utafiti huo katika jarida la
'Epidemiology and Community Health',unasema kuwa shughuli za kukidhi
matakwa na mahitaji ya jamii pia zimehusishwa na idadi kubwa ya vifo vya
mapema.
Pia kulingana na utafiti huo utu wa mtu na uwezo wa mtu binafsi kukabiliana na dhiki ilichangia katika matokeo ya utafiti huo.
Ingawa watafiti hao kutoka chuo kikuu cha
Copenhagen waliweza kupata uhusiano uliopo kati ya vifo vya mapema na
kugombana, na kuwa ugomvi uliongeza hatari ya vifo vya mapema mara tatu,
hawakuweza kuelezea kikamilifu sababu haswa ya hali hiyo.
Utafiti wa hapo awali ulionyesha kuwa watu wenye
wasiwasi mwingi na mahitaji mengi kutoka kwa wapenzi wao na watoto,
pamoja na wale wanao gombana mara kwa mara na jamaa wao, wamo katika
hatari kubwa zaidi ya kuugua magonjwa ya moyo na kiharusi.
Tafiti za hapo awali pia zaonyesha kuwa
utangamano mwema na watu pamoja na marafiki wengi ina athari chanya
katika afya, huku utu kwa kiasi kikubwa ukiamua jinsi mtu hupokea na
kuguswa na hali za kijamii pamoja na mahusiano.
Wapendanao hawapaswi kugombana
Katika utafiti huu, watafiti walisema kuwa athari za kisaikolojia
zinazosababishwa na dhiki, kama vile shinikizo la damu na ongezeko la
athari ya magonjwa ya moyo, ndizo hasa zinaweza kueleza athari ya
ongezeko la vifo vya mapema.
Utafiti umeonyesha kuwa wanaume wanapokabiliwa
na hali za dhiki kwa kuongeza homoni inayokabiliana na hali ya dhiki na
wasiwasi, jambo ambalo linazidisha athari ya kiafya.
Utafiti huo ulihusisha watu 9,875 wake kwa waume
wenye umri wa kati ya miaka 36 na 52 na ulitumiwa kuchunguza uhusiano
uliopo baina ya hali ngumu ya uhusiano wa kijamii na vifo vya mapema.
Wote walikuwa wameshiriki katika Utafiti ‘Denmark Longitudinal’ kuhusu Ajira, ukosefu wa ajira na afya , kuanzia mwaka wa 2000.
Utafiti uligundua kuwa wasiwasi wa mara kwa mara
au mahitaji yanayotokana na wapenzi na watoto ulihusishwa na ongezeko
la kufikia 50%- 100% la vifo vya mapema.
Ukosefu wa ajira ulionekana kuongeza athari hasi
za uhusiano mgumu wa kijamii. Wale ambao hawako kazini wameonekana kuwa
katika hatari kubwa zaidi ya kifo kutokana na jambo lolote kinyume na
wale walio na kazi.
wanaume pia wako katika hatari zaidi kutokana na
mahitaji na wasiwasi unaotokana na wapenzi wao wa kike , huku wakiwa
katika hatari kubwa zaidi ya kifo zaidi ya ile ambayo kwa kawaida
imehusishwa na kuwa mwanamume.
Dakta Rikke Lund, wa kitengo cha afya ya u,mma
katika chuo kikuu cha Copenhagen amesema kuwa wasiwasi na ugomvi ni
sehemu ya maisha. Lakini akaongeza kuwa watu ambao wanakuwa na migogoro
mara kwa mara wako katika hatari zaidi lakini wanaweza wakasaidiwa.





0 comments:
Chapisha Maoni