Serikali imesema itafanya maboresho ya Daftari la Kudumu la
Wapiga Kura kwa awamu mbili kabla ya upigwaji wa kura ya maoni kupitisha
Katiba Mpya.
Uamuzi huo wa Serikali unafanyika ikiwa imepita
miaka mitano tangu Daftari hilo lilipoboreshwa mara ya mwisho Machi
2009, kabla ya kufanyika kwa uchanguzi Mkuu mwaka 2010.
Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) inatakiwa kuboresha daftari hilo mara mbili kati ya
uchaguzi mkuu mmoja na unaofuata, pia imebainisha kuwa itaboresha
daftari hilo kwa mfumo wa Biometric.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi wakati akiwasilisha
rasimu ya mapendekezo ya bajeti ya ofisi yake kwa Kamati ya Katiba na
Sheria.
Lukuvi alisema NEC imepanga kuboresha daftari hilo
kwa awamu mbili kwa mfumo huo ili kuweza kuondoa changamoto
zilizojitokeza katika mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition(OMR).
Alisema awamu ya kwanza ya maboresho hayo, itaanza
Septemba hadi Desemba, kwa tume kuandikisha watu wote upya, pamoja na
watakaotimiza umri wa kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwakani.
Hatua hii itatekelezwa wakati mchakato wa Katiba
ukiendelea kwa Bunge Maalumu la Katiba kujadili Rasimu hiyo kwa siku 60
kuanzia Agosti 5, kisha itafuatiwa na mchakato wa kura ya maoni ambao
utawapa nafasi wananchi walioingizwa katika daftari hilo kushiriki
kuipigia kura.
Waziri Lukuvi alisema awamu ya pili inatarajiwa
kufanyika kati ya Aprili hadi Agosti mwakani, ambapo itahusisha
wapigakura waliohama toka sehemu moja kwenda nyingine, kuwaondoa
wapigakura watakaokuwa wamefariki au kupoteza sifa na wapiga kura
watakaokuwa wamepoteza kadi au kadi zao kuharibika.
0 comments:
Chapisha Maoni