WAKATI fainali za Kombe la Dunia zikiwa zinakaribia kuanza,
vioja mbalimbali vimeanza kuibuka kutokana na maombi mbalimbali
yanayowasilishwa na baadhi ya timu katika masharti ya kushiriki fainali
hizo.
Ronaldo kulindwa na mabaunsa sita
Shirikisho la Soka la Ureno limeomba walinzi sita
kwa ajili ya safari zao mbalimbali za kujiburudisha miili yao katika
fukwe za Copacabana na kwingineko. Kati ya walinzi wao, wanne watakuwa
na kazi ya kumlinda Mwanasoka Bora wa Dunia kwa sasa, Cristiano Ronaldo
peke yake wakati wengine watakuwa na kazi ya kulinda wachezaji wengine
na viongozi wa timu hiyo. Ronaldo, Lionel Messi na Neymar wanatarajiwa
kuwa mastaa wenye mvuto zaidi katika michuano hiyo kutokana na ubora wao
katika ligi mbalimbali za Ulaya.
Ufaransa wataka sabuni za maji
Katika hali ya kushangaza, Ufaransa ambao
wataongozwa na wakali kama Franck Ribery, Olivier Giroud, Karim Benzema
na wengineo wametoa madai ya kushtusha zaidi baada ya kudai kwamba
watataka sabuni za maji katika vyumba vya wachezaji wao na si sabuni za
vipande.
Uongozi wa mabingwa hao wa Kombe la Dunia mwaka
1998 wanataka vyumba vyao vyote vya hoteli watakayofikia jijini Sao
Paulo kuwekwa sabuni za maji na sio sabuni za vipande. Ufaransa pia
wanataka hoteli yao iwe na nyama ambazo zimechinjwa kihalali kwa sababu
wachezaji wao wengi ni Waislamu.
Akina Valencia wataka ndizi zao
Timu ya taifa ya Ecuador imeandika maombi yao ya
kutaka kila mchezaji wao apewe kikapu cha ndizi mbivu kutoka nchini kwao
Ecuador kila siku ya michuano hiyo. Kikosi chao kinachoongozwa na mkali
wa Manchester United, Antonio Valencia kinataka ndizi hizo zisafirishwe
kutoka katika ardhi ya kwao Ecuador kila siku. Ndizi mbivu ni chakula
maarufu kwa wanasoka wote duniani kwa ajili ya kurudisha sukari
iliyopotea mwilini kutokana na mazoezi mazito ya kila siku.
Algeria wataka Kurani kila chumba
Shirikisho la Soka la Algeria limetaka kila chumba
cha wachezaji pamoja na maofisa watakaoambatana na timu hiyo kuwekwa
vitabu vitakatifu vya dini ya Kiislamu, Kurani kwa ajili ya maombi yao
ya kila siku wakati watakapokuwa katika michuano hiyo. Kikosi chote cha
Algeria kitakuwa na wachezaji Waislamu. Hapana shaka baadhi ya wachezaji
wakubwa duniani wanaofuata imani ya Kiislamu ambao watakuwa katika
michuano hiyo wanaweza kuhitaji pia kuwekewa Kurani katika vyumba vya
hoteli zao. Wachezaji hao ni kama Mesut Ozil, Yaya Toure, Cheikh Tiote,
Samir Nasri na wengineo.
Australia wameomba katika hoteli yao kuwe na vyumba maalumu vya
kahawa kwa ajili ya wachezaji wao. Wanataka pia katika vyumba hivyo
maalumu kwenda na magazeti mbalimbali kutoka pembe zote za dunia kwa
ajili ya kupata habari na kuburudika. Mastaa wao ambao wanataka kupoza
vichwa kwa kahawa na magazeti ni pamoja na kiungo wa zamani wa Everton,
Tim Cahill anayekipiga na Thierry Henry katika klabu ya New York Red
Bull pamoja na kipa, Mark Schwarzer anayekipiga Chelsea akiwa msaidizi
wa Petr Cech.
Chile wataka vitanda vipya
Mastaa wa Chile ambao hapana shaka wataongozwa na
mkali wa Barcelona, Alexis Sanchez pamoja na David Pizarro wa Bayern
Munich, Arturo Vidal na Mauricio Isla wa Juventus wametaka kila chumba
watakachofikia kiwe na kitanda kipya pamoja na seti mpya za televisheni.
Wametaka vitanda vya zamani vyote viondolewe pamoja na seti za zamani
za televisheni ziondolewe.
Colombia waja na kali mpya
Shirikisho la Soka la Colombia limekuja na kali
mpya. Wanataka wachezaji 15 wa timu ya vijana ya Sao Paulo wapelekwe
katika kambi yao kwa ajili ya kucheza mechi za kirafiki za mazoezi kila
siku asubuhi. Wanataka mazoezi yao yawe ya nguvu na itakuwa vigumu
kupata kitu hicho kama watacheza wenyewe kwa wenyewe. Colombia ipo Kundi
C pamoja na Ugiriki, Ivory Coast na Japan.
Honduras wataka TV za Kihispaniola
Shirikisho la Soka la Honduras linataka stesheni
sita za idhaa za Hispania ziongezwe katika televisheni za vyumbani kwao
huku pia wakitaka idhaa mbili za Honduras nazo ziongezwe katika idhaa za
hoteli hiyo. Madai yao ni kama ya timu ya taifa ya Uswisi ambao
wanataka kuwe na chaneli mbili za televisheni za kwao Uswisi katika kila
chumba.
Wakati wao wakitaka madai hayo yatimizwe, Japan
wanataka kila chumba kiwe na bafu la fahari la kuogea, Jacuzzi kwa ajili
ya kuhakikisha wachezaji wao wanapumzika vilivyo baada ya mazoezi na
mechi zao.
Ni kama ilivyo kwa Luis Suarez na Uruguay yao ambapo wamekuwa wakitaka kuwa na vipoza hewa (Air Conditions) zisizotoa sauti.
Video games zatawala
Maombi yaliyotumwa na timu nyingi zaidi kwa pamoja
ni yale ya kutaka kuwepo kwa vyumba vya michezo ya kompyuta (Video
games). Ufaransa, Ecuador na Costa Rica zote zimepeleka maombi hayo,
lakini Ureno inataka kila chumba cha hoteli yao kiwe na Video Game.
0 comments:
Chapisha Maoni