Kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika MISCA
kilichoko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kimetangaza vita dhidi ya
wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka ambao wamekuwa wakiwauwa kinyama
Waislamu wa nchi hiyo.
Hatua hiyo ni radiamali ya vikosi hivyo baada ya askari wake
kushambuliwa na wanamgambo hao. Jenerali Jean Marie Michel Mokoko,
kamanda wa kikosi cha MISCA katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ametangaza
kuwa, kuanzia sasa wanawahesabu wanamgambo wa Anti Balaka kuwa ni maadui
wao na watahakikisha wanakabiliana nao vilivyo. Kikosi hicho cha Umoja
wa Afrika kimekuwa kikipambana na wanamgambo wa Anti-Balaka katika mji
mkuu Bangui tangu siku ya Jumamosi ambapo kwa uchache watu 16
wanaripotiwa kuuawa katika mapigano ya hivi karibuni kabisa nchini humo.
Wakati huo huo, Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International
limetoa wito wa kutumwa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Ulaya
huko Jamhuri ya Afrika ya Kati. Taarifa ya Amnesty International
imebainisha kwamba, hali ya mambo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
inatia wasi wasi kwani wanamgambo wa Anti-Balaka kila siku wamekuwa
wakidhibiti maeneo zaidi katika mji mkuu Bangui na kuendelea kufanya
mauaji.
0 comments:
Chapisha Maoni