Jumanne, Machi 04, 2014

OBAMA AZUA JIPYA

Rais Obama ametangaza mapendekezo ambayo huenda yakatoa suluhu kwa mzozo wa Ukraine, ikiwemo kuwatuma wachunguzi wa kimataifa na kuanzishwa mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Moscow na serikali mpya mjini Kiev.
Bwana Obama amejadili swala hilo kwa njia ya simu na chanzela wa Ujerumani, Angela Merkel.

Wachunguzi hao watalenga kulinda haki za watu wa kabila la Urusi waliopo katika jimbo la Crimea; na kwa upande wake Urusi itahitajika kuwaondoa wanajeshi wake katika jimbo hilo. Pendekezo hilo huenda likajadiliwa pembezoni mwa mkutano utakaofanyika nchini Ufaransa (Jumatano) ambao utawaleta pamoja wajumbe kutoka Marekani, Urusi na kwingineko kwa ajili ya kuijadili Lebanon.
Hapo awali waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Marekani John Kerry, amelaani kile amekitaja kuwa kitendo cha uchukozi kutoka Urusi dhidi ya Ukraine. Wakati wa ziara yake mjini Kiev ambapo aliweka shada la maua kuwakumbuka waandamanaji waliouwawa mwezi uliopita, bwana Kerry ameshutumu Moscow kwa kutumia uongo na vitisho kuficha ukweli.
Mwandishi wa BBC Sarah Reinsford aliyepo mjini Kiev amesema kuwa wakati akiweka shada la maua katika maeneo walikouwawa mamia ya waandamanaji mjini humo, John Kerry alikaribishwa na umati wa watu waliokuwa wakiomba msaada wa marekani.
Na hilo ndilo lililomleta hapa; kutoa msaada wa hali na mali na pia wa kisiasa kwa serikali ya mpito ya Ukraine, na pia ahadi ya msaada wa kifedha na wa kiufundi kusaidia katika kuimarisha uchumi, amesema mwandishi wetu.

0 comments:

Chapisha Maoni