Serikali imemvua wadhifa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii nchini (TTB), Dk Aloyce Nzuki kutokana na utendaji usioridhisha.
Akitangaza uamuzi huo jana mbele ya waandishi wa
habari, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alisema kuwa
ameridhia uamuzi wa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo ambao
walipendekeza mkurugenzi huyo aondolewe.
Katika barua waliyomwandikia Waziri ikiwa
imesainiwa na Mwenyekiti wa Bodi, Charles Sanga na kuridhiwa na wajumbe
wote, walidai Nzuki alishindwa kuutangaza utalii ambalo ndilo jukumu la
bodi hiyo.
“Nilipata barua kutoka TTB ikinishauri kumwondoa
Bwana Nzuki na baada ya kushauriana na naibu wangu na katibu mkuu
nikaona ni vyema kukubaliana na ushauri wa bodi,” alisema Nyalandu jana,
huku akiwa na naibu wake, Mahamoud Mgimwa na wajumbe wa Bodi ya TTB.
Nyalandu alisema Dk Nzuki atapangiwa kazi nyingine ndani ya wizara hiyo .
Aliwaomba Watanzania wenye uwezo kuomba nafasi
hiyo hata wale walio nje ya nchi ili kuweza kusaidia kukuza utalii wa
nchi, uwe mbele ya mataifa mengine duniani.
“Nategemea katika siku 21 nafasi hiyo iwe
imezibwa, kwani nimewashauri watumie kampuni inayoheshimika ili kufanya
mchakato huo ,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya mchujo kufanyika, bodi
hiyo itampa majina ya watu watatu ambayo baadaye atayapeleka kwa Rais
Jakaya Kikwete kwa ajili ya moja kuteuliwa kujaza nafasi hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni