Wakati Serikali ya Malaysia imenawa mikono kuwa imeshindwa
kuipata ndege yake iliyopotea ikiwa na abiria 239 na wafanyakazi 12,
ripoti ya ajali za ndege hapa nchini inabainisha kuwa tangu mwaka 1920
hadi 2013 zimewahi kutokea ajali 52 zilizosababisha vifo vya watu 196.
Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege nchini, kutoka
Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi, David Nyamwihura alisema katika
mahojiano maalumu kuwa ripoti hiyo inaonyesha kuwa idadi kubwa ya ajali
hizo hutokea maeneo ya milimani.
“Ukiangalia ripoti hii utaona ndege nyingi
zinaanguka maeneo ya milimani, sababu kubwa ni hali mbaya ya hewa na
ukosekanaji wa vyombo vya kuangalia hali ya hewa,” alisema Nyamwihura.
Ripoti hiyo imeorodhesha ajali za ndege kulingana
na idadi ya watu waliokufa, mahali ilipotokea na aina ya ndege
iliyohusika, kuanzia na yenye wingi mkubwa wa vifo.
DC -3- Machi 18, 1955
Hii ndiyo ajali mbaya zaidi ya ndege kuwahi
kutokea katika anga la Tanzania, ikihusisha ndege DC-3 ya Shirika la
Ndege ya Afrika Mashariki. Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mlima
Kilimanjaro na kuua watu 20.
Vickers Viking-Machi 29, 1953
Ajali ya pili ni ile iliyohusisha ndege aina ya
Vickers Viking mali ya Shirika la Ndege la Afrika ya Kati iliyotokea
eneo la Mkuyuni, Handeni ambapo watu 13 walifariki dunia.
Cessna 404-Septemba 9, 1999
Hii ni ya tatu ambayo ilihusisha ndege ya Shirika
la Northern Air, aina ya Cessna 404. Ajali hiyo iliyotokea eneo la Mlima
Meru, Arusha, ilisababisha vifo vya watu 12.
Cessna 402b-Agosti 12, 1976
Ripoti hiyo inabainisha kuwa ajali ya nne ilikuwa
ya ndege aina ya Cessna 402B ya Shirika la Safari la Air Nairobi. Ajali
hiyo iliyotokea katika Ziwa Victoria, Mwanza, watu 10 walipoteza maisha.
IL76-TD Machi 23-2005
IL76-TD Machi 23-2005
Ajali ya tano kwa wingi wa vifo, iliua watu wanane
katika Ziwa Victoria, mkoani Mwanza. Ilihusisha ndege aina ya IL76-TD,
mali ya Shirika la Air Trans Inc, Moldova.
Piper PA 32-300 Agosti 26, 1972
Ajali ya sita ni ile ya ndege aina ya Piper PA
32-300 inayomilikiwa na Shirika la Ndege la K. Downey and Selby la
Nairobi iliyoanguka katika anga la Dar es Salaam eneo la Kijiji cha
Mkamba. Watu saba walipoteza maisha.
Piper PA 32-300 Agosti 15, 1978
Ajali namba saba ilihusisha ndege aina ya Piper PA
32-300 mali ya Shirika la Amphibian Mombasa. Katika ajali hiyo
iliyotokea eneo la Tarakea, Mlima Kilimanjaro, watu saba walipoteza
maisha.
Piper PA 23-250 Machi 30, 1970
Mwaka 1970 nao ulishuhudia ajali ya nane kwa
ukubwa ya ndege aina ya Piper PA 23-250 mali ya Shirika la Tim Air,
Tanzania katika eneo la Mafi Hill, Mombo ambapo watu sita walipoteza
maisha.
Piper PA 23-250 Juni 2, 1979
Ajali ya tisa iliyotokea Juni 2, 1979,
ilisababisha vifo vya watu watano na ilitokea eneo la Kambi ya Jeshi la
Mgambo, Tanga. Ajali ilihusisha ndege aina ya Piper PA 23-250 mali ya
Shirika la Tanzanair, Dar es Salaam.
Cessna 185-Oktoba 10, 1986
Ajali ya 10 mbaya zaidi ni ya mwaka 1986
iliyotokea katika eneo la Hombolo, Dodoma, ambapo ndege ya Shirika la
NORAD, aina ya Cessna 185 ilianguka na kusababisha vifo vya watu watano.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, hizo si ajali pekee zilizowahi kutokea nchini, zipo nyingine zilizotokea mwaka 1986, 1988, 1998 na 2005 ambazo ziliua watu watano kila moja.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo, hizo si ajali pekee zilizowahi kutokea nchini, zipo nyingine zilizotokea mwaka 1986, 1988, 1998 na 2005 ambazo ziliua watu watano kila moja.
Hali kadhalika miaka ya 1965, 1990, 2006 na mwaka 2008 ilishuhudia ajali nne za ndege zilizopoteza roho za watu wanne kila moja.
Pia miaka ya 1969, 1970, 1976, 1979 na 1984, 1995,
1990, 1998 na 2008 nayo ilishuhudia ajali tisa za ndege ambazo kila
moja iliua watu watatu.
Ripoti hiyo pia inadokeza zaidi kuwa, miaka ya
1984, 1994, 2003, 2008, na 2010 nayo ilishuhudia ajali za ndege sita
ambazo kila moja ilisababisha vifo vya watu wawili.
Pia, ripoti hiyo inaweka wazi kuwa, miaka ya 1992,
1995, 1996, 1997, 2007, 2011 2013, 1950, 1931, 1969, 1970, 1972, 1973,
1980, 1985 na 1990, ajali kadhaa zilitokea na kusababisha kifo cha mtu
mmoja mmoja, wengi wakiwa ni marubani.
0 comments:
Chapisha Maoni