Korea Kaskazini imefanyia majaribio makombora mawili ya
masafa ya kati kwa kuyavurumisha katika pwani ya bahari upande wa
mashariki kuelekea Japan.
Hayo yamejiri masaa machache baada ya viongozi wa Korea Kusini, Japan
na Marekani kukutana huko Uholanzi kujadili mipango ya nyuklia ya
Pyongyang.
Hii ni mara ya kwanza Korea Kaskazini kufanyia majaribio makombora ya
aina hiyo tangu mwaka 2009, hatua inayoonesha kupiga hatua nchi hiyo
kutoka makombora ya masafa mafupi ambayo imekuwa ikiyarusha katika wiki
za hivi karibuni.
Marekani na Korea Kusini zimelaani majaribio hayo ambapo naibu
msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Marie Harf ameitaka Korea
Kaskazini kusitisha majaribio hayo na kuacha hatua za vitisho. Naye
msemaji wa Korea Kusini Kim Min-seok ameeleza kuwa, makombora hayo yana
uwezo sio tu wa kulenga Japan bali pia Russia na China.
Katika wiki za hivi karibuni Korea Kaskazini imefanyia majaribio
makombora kadhaa ya masafa mafupi, hatua iliyokwenda sambamba na
kufanyika manuva ya pamoja ya kijeshi ya kila mwaka kati ya Korea Kusini
na Marekani.
0 comments:
Chapisha Maoni