Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Amnesty International limesema
wakimbizi Wasomali walioko Kenya wanadhulumiwa na haki zao kukiukwa,
jambo ambalo linawalazimisha kuondoka katika nchi hiyo.
Katika ripoti iliyochapishwa Jumatano, shirika hilo la kutetea haki
za binadamu limeonya kuhusu mazingira mabaya ya wakimbizi Wasomali
nchini Kenya na kusema wanabughudhiwa na polisi na kukamatwa kiholela
bila sababu yoyote ya kisheria. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa
anwani ya ‘No Place Like Home’ au ‘Hakuna Pahala Bora Zaidi ya
Nyumbani’, Amnesty imesema wakimbizi wananyimwa haki ya msingi ya
usajili na hilo linamaanisha kuwa wanaishi kinyume cha sheria nchini
Kenya. Naibu Mkuu wa Amnesty International mashariki mwa Afrika Sarah
Jackson amesema wakimbizi Wasomali huko Kenya wana hali mbaya sana na
kwa hivyo hawana budi ila kurejea makwao. Amesema kuyafanya mazingira
yawe magumu kiasi cha kutoweza kustahimilika ni sawa na kuwalazimisha
kurejea katika nchi yao ambayo bado inakumbwa na vita.
Wiki iliyopita serikali ya Kenya ilitoa wito kwa Somalia kuharakisha
mchakato wa kuwapokea karibu wakimbizi nusu milioni wa Kisomali
wanaoishi katika kambi za Umoja wa Mataifa nchini Kenya. Serikali ya
Somalia imeafiki suala hilo lakini inasema wakimbizi wanapaswa
kurejeshwa hatua kwa hatua.
0 comments:
Chapisha Maoni