Serikali ya Afrika Kusini imesimamisha utoaji viza kwa raia wa
Kinyarwanda wanaotaka kuingia nchini humo. Taarifa iliyotolewa leo na
ubalozi wa Afrika Kusini ulioko mjini Kigali imeeleza kuwa, tokea tarehe
10 Machi serikali ya Pretoria imesimamisha utoaji viza kwa raia wa
Kinyarwanda wanaotaka kufanya safari nchini Afrika Kusini. Naye Louise
Mushikiwabo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Rwanda amesisitiza kuwa,
Kigali imesikitishwa na hatua ya serikali ya Afrika Kusini ya
kuwahifadhi wahusika wa mashambulio ya kigaidi yaliyofanyika nchini
Rwanda. Mgogoro kati ya pande hizo mbili ulianza hivi karibuni, baada ya
serikali ya Afrika Kusini kuwatimua wanadiplomasia watatu wa Rwanda,
nayo serikali ya Kigali ikaamua kulipiza kisasi kwa kuwafukuza
wanadiplomasia sita wa Afrika Kusini waliokuwa Kigali. Wanadiplomasia
hao wanatuhumiwa kuhusika na mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na
waasi wa serikali ya Rwanda walioko uhamishoni Afrika Kusini. Imeelezwa
kuwa, uhusiano wa pande hizo mbili umekuwa ukilegalega katika miaka ya
hivi karibuni, baada ya Afrika Kusini kupeleka majeshi yake mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa shabaha ya kulinda amani,
kitendo ambacho kinaonekana kuikasirisha serikali ya Kigali.
0 comments:
Chapisha Maoni