Wosia wa aliyekuwa Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini,
Nelson Mandela umesomwa huku mgawanyo wa mali zake ukielekezwa katika
maeneo tofauti.
Katika wosia huo uliosomwa rasmi jana, Mandela
aliacha mali zenye thamani ya Dola za Marekani 4.1 milioni, sawa na
Sh5.6 bilioni ambazo zimepangwa kugawiwa kwa taasisi mbalimbali, familia
na wafanyakazi wake.
Katika wosia huo ulioandikwa na Mandela mwenyewe
mwaka 2004 na kufanyiwa marekebisho mwaka 2008, mkewe, Graca Machel
anapata karibu nusu ya mali zake zote alizoziacha.
Mali hizo zinajumuisha nyumba kubwa alizokuwa
akimiliki moja ikiwa Johanesburg, nyingine Qunu na ya tatu Mthatha. Mali
nyingine ni sehemu ya mrabaha aliyokusanya baada ya kuuza machapisho
mbalimbali ikiwamo kitabu chake maarufu cha “Long Walk to Freedom”
ambacho kinatajwa kuuzwa kwa wingi duniani.
Pia sehemu za mali hizo zimetokana na kazi
mbalimbali alizozifanya wakati akiwa rais na baada ya kuachia madaraka
na kujihusisha na wakfu wake wa Mandela Foundation. Wakfu huo ndiyo
uliofanikisha kuratibu shughuli mbalimbali za kijamii ambazo
alizitekeleza baada ya kustaafu.
Kutangazwa kwa mali hizo kumemaliza minong’ono ya
muda mrefu iliyokuwa ikihusisha sehemu kubwa ya familia yake ambayo
imewahi kuingia kwenye malumbano juu ya nani anayepaswa kumiliki mali
hizo.
Akisoma wosia ulioachwa na Mandela mbele ya
waandishi wa habari, Naibu Jaji Mkuu Dikgang Moseneke alisema
wanafamilia ya Mandela wamekubaliana na yote yaliyoandikwa na hakuna
pingamizi lolote lililotijokeza.
Hata hivyo, kuna nafasi ya kuweka pingamizi juu ya
wosia huo katika kipindi cha siku 90 kuanzia sasa vinginevyo, baada ya
hapo utaanza kutekelezwa mara moja.
Wosia huo uliokuwa na kurasa 40 umeorodhesha watu
na taasisi zinazostahili kuwa sehemu ya mgawanyo huo wa mali na kutaja
kiwango stahili kinachopaswa kutolewa.
Chama cha ANC ambacho Mandela na marafiki zake
walikiasisi kwa ajili ya kukabiliana na siasa za kibaguzi wakati wa
utawala wa makaburu ni miongoni mwa taasisi ambazo zitapitiwa na mgawo
huo.
Kamati Kuu ya ANC inatazamia kutumia fedha hizo kwa ajili ya kusambaza sera na misingi ya chama inayohusu maridhiano.
Wengine waliotajwa kwenye urithi huo ni pamoja na
aliyekuwa msaidizi wake katika siku zake za mwisho, Zelda la Grange,
Chuo Kikuu cha Wits, Shule ya Sekondari ya Qunu na Shule ya Sekondari ya
Orlando iliyoko Soweto.
0 comments:
Chapisha Maoni