Ijumaa, Desemba 13, 2013

HIZI NDIO TIMU 16 ZA HATUA YA MTOANO KATIKA UEFA

Timu 16 zitakazomenyana katika hatua ya mtoano ya mashindano ya soka ya Klabu Bingwa barani Ulaya zilikamilika jana kwa mechi kadhaa zilizofanyika katika viwanja tofauti.
Timu ya Barcelona na Uhispania ambayo ilikuwa tayari imejihakikishia kushiriki awamu ya mtoano iliinyuka Seltic ya Scotland mabao 6 kwa moja baada ya mshambuliaji machachari wa Barca Meymar kung'ara katika mechi iliyochezwa uwanja wa  Camp Nou. Neymar alipachika magoli matatu kati ya sita na kuigaragaza Celtic.
Arsenal ya Uingereza imeingia pia katika raundi ya mtoano licha ya kupigwa mabao mawili kwa nunge na Napoli ya Italia ikiwa ugegeni. Katika kundi hilo The Gunners wameingia raundi ya pili kwa kuwa na pointi 12 nyuma ya Borussia Dortmund ya Ujerumani ambayo nayo ina pointi 12.

Bibi Kizee wa Torino, Juventus imeaga mashindano ya Klabu Bingwa barani Ulaya baada ya kupigwa goli moja na Galatasaray ya Uturuki. Juve ilihitaji kutoka sare ili iweze kuendelea na mashindano hayo lakini goli la dakika ya 85 la mchezaji la Wesley Sneijder katika dimba la Türk Telekom Arena mjini Istanbul limeua ndoto ya Juve na kocha wake Antonio Conte.
AC Milan pia imefanikiwa kuingia raundi ya mtoano na kuwasitiri Wataliano ambao timu zao mbili za Juve na Napoli ziliaga mashindano hayo jana kwa kutoka sare ya bila ya kufungana na Ajax ya Uholanzi na Chelsea imefanikiwa kusonga mbele kwa kuilaza Steaua Bucharest bao moja kwa nunge.

0 comments:

Chapisha Maoni