Jumanne, Septemba 17, 2013

JAMAA AKAMATWA NA SILAHA HATARI MBEYA

Wakati zoezi la kuwakamata wahamiaji haramu na watu wanaomiliki silaha kinyume na sheria likiendelea nchini kwa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dakta Jakaya Mrisho Kikwete, Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya linamshikilia Sebastian Marcus baada ya kumkuta na silaha kinyume cha sheria katika kitongoji cha Kibete – Mkunywa, wilayani Mbalali katika mkoa wa Mbeya . 
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa sita usiku wakati Askari Polisi wakiwa doria walipomkamata mtuhumiwa Sebastian Marcus, 36, Mhehe na mkazi wa Igoma katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa akiwa silaha moja, Bunduki aina ya MARK IV NO. BX-10400 na risasi mbili pasipokuwa na kibali. 
Mbinu aliyoitumia mtuhumiwa ni kuificha silaha hiyo katika mfuko wa sandarusi na kupakia katika baiskeli na taratibu za kumfikisha mtuhumiwa mahakamani zinaendelea. 
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi wa jeshi la polisi Diwani Athumani anatoa wito kwa jamii kuacha kumiliki silaha bila kibali kwani ni kinyume cha sheria . Pamoja na hilo, anatoa wito kwa yeyote aliye taarifa juu ya mtu au watu wanaomiliki silaha isivyo halali azitoe kwa katika mamlaka husika ili hatua za kisheria zichukuliwe.

0 comments:

Chapisha Maoni