Jumanne, Septemba 17, 2013

WATU WAWILI WAMEUAWA KATIKA MATUKIO TOFAUTI MBEYA

Watu wawili wamefariki dunia katika matukio mawili tofauti mkoani Mbeya jana katika wilaya za Mbeya vijijini na Momba katika majira tofauti. 

Katika tukio la kwanza, Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuchomwa na kisu tumboni jana majira ya saa kumi jioni huko katika kijiji cha Isuto-Mlowo, wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya. 
Marehemu amefahamika kwa jina la Boaz Samsoni, 25, Mmalila, mkulima na mkazi wa kijiji cha Isuto ameuawa kwa kuchomwa kisu tumboni na mtu aliyefahamika kwa jina la Bakel Msafiri, 
Chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana na bado kinachunguzwa na makachero wa polisi lakini uchunguzi wa awali unaonesha kuwa ni kudhurumiana katika mchezo wa kamari kati ya mtuhumiwa na marehemu, wakati mwili wa marehemu umehifadhiwa katika zahanati ya kijiji cha Isuto. 
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi wa jeshi la polisi Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa yeyote aliye na taarifa juu ya mahali alipo mtuhumiwa azitoe katika mamlaka husika ili sheria ifuate mkondo wake ama ajisalimishe mwenyewe, ni kutokana na mtuhumiwa kukimbia baada ya tukio. 
Katika tukio la pili, mtu mmoja amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea jana majira ya saa moja asubuhi katika eneo la Mpemba, barabara ya Tunduma/Mbeya, katika wilaya ya Momba mkoani Mbeya. 
Habari zinaeleza kuwa ajali hiyo iliyohusisha gari na dereva asiyefahamika lilimgongampanda pikipiki Cernain Silungule, 22, Mnyamwana na mkazi wa mpemba na kusababisha kifo chake papo hapo. 
Maafisa wa polisi wamesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa mwendesha gari. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya Tunduma na dereva alikimbia na gari baada ya kusababisha ajali hiyo. 
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi wa jeshi la polisi Diwani Athumani ametoa wito kwa madereva kuwa makini waendeshapo vyombo vya motokwa kuzingatia sheria za usalama wa barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika. Aidha ametoa rai kwa yeyote aliye na taarifa juu ya mahali alipo mtuhumiwa na gari azitoe ili akamatwe ili hatua za kisheria zichukuliwe au ajisalimishe.

0 comments:

Chapisha Maoni