Chama cha Movement for Democratic Change (MDC) nchini Zimbabwe kimewasilisha malalamiko yake mahakamani kupinga ushindi wa Robert Mugabe katika uchaguzi wa rais wa wiki iliyopita.
MDC inataka matokeo ya uchaguzi huo yabatilishwe na uchaguzi mpya uitishwe katika kipindi cha siku 60. Chama hicho kimetaja mambo 15 ,mkiwemo madai ya kutoa hongo,kutumia vibaya haki ya kuwasaidia wapigaji kura na kuvuruga daftari za wapiga kura. Bw Mugabe,mwenye umri wa miaka 89, alishinda uchaguzi kwa asilimia 61% ya kura.
Chama chake cha Zanu-PF kilipata zaidi ya theluthi mbili za viti vya bunge ikishinda viti 160 ikilinganishwa na viti 49 kwa MDC.
Mawakili wa MDC,waliowasilisha malalamiko yao katika mahakama ya katiba,wameiambia BBC kwamba walikuwa na ushahidi thabiti wa kutumika mbinu zisizo za kawaida katika utaratibu wa upigaji kura. Walisema idadi kubwa ya watu hawakuweza kupiga kura na kwamba chakula chakula na vitu vingine vilitumika kama hongo za kuwashawishi wapigaji kura wampigie kura Bwana Mugabe. "Chama cha Movement of Democratic Change kinataka matokeo ya uchaguzi huu yatenguliwe kuwa batili kwa mujibu wa ibara ya 93 ya katiba ya Zimbabwe"Amesema msemaji wa MDC Douglas Mwonzora. Hatua ya MDC inakuja baada ya tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kusema takriban wapigaji kura 305,000 walikataliwa kupiga kura siku ya uchaguzi.
0 comments:
Chapisha Maoni