Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Kumekuwa na tukio 01 la taarifa ya kifo kama ifuatavyo:-
Mnamo tarehe 16.01.2017 majira ya saa 10:30 Asubuhi huko Igoma “A”, Kata ya Isanga, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilipokea taarifa kuwa maiti iliyokwenda kuzikwa katika makaburini ya zamani ya Isanga kukutwa nyumbani, chumbani ikiwa kwenye godoro.
Kufuatia taarifa hiyo Polisi walifuatilia na kubaini kuwa tarehe 16.01.2017 majira ya saa 07:00 Asubuhi Mtu mmoja aitwaye JAILO KYANDO [36] Muosha magari na mke wake aitwaye ANNA ELIEZA [32] wote wakazi wa Mtaa wa Igoma “A” waliamka asubuhi na kukuta mtoto wao wa kwanza aitwaye HARUN JAILO KYANDO [09] amefariki dunia akiwa amelala.
Taarifa za awali zinadai kuwa marehemu tangu utoto wake alikuwa na matatizo ya ugonjwa wa kifafa hali iliyopelekea kuishi nyumbani pasipo kusoma. Kufuatia kifo hicho msiba uliendeshwa na taratibu za mazishi zilifanyika. Majira ya saa 12:00 Mchana jeneza lililoletwa msibani na kuwekwa sebuleni kando ya mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeviringishwa na blanketi na kulazwa chini kwenye godoro, baada ya maombi yaliyoongozwa na walokole waitwao BONDE LA BARAKA vijana walibeba jeneza hadi makaburi ya zamani ya Isanga na kisha jeneza kuzikwa.
Waombolezaji waliporudi nyumbani walitaharuki kuona mwili wa marehemu Mtoto HARUN JAILO KYANDO ukiwa chumbani umelazwa eneo ulipokuwa awali. Kutokana na hali hiyo taarifa zilifikishwa Polisi mara moja, askari Polisi walifika na kurejesha hali ya amani kwa kuuchukua mwili wa marehemu ambao kwa sasa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.
Taratibu nyingine za mazishi zitafanyika leo tarehe 17.01.2017. Mpaka sasa bado haijafahamika ni uzembe /bahati mbaya wafiwa kusahau kuweka mwili wa marehemu kwenye jeneza au kulikuwa na hujuma zozote. Upelelezi unaendelea kuhusiana na tukio hili.
0 comments:
Chapisha Maoni