Jumamosi, Mei 14, 2016

KWANINI KINGO ZA MABAWA YA NDEGE HUELEKEA JUU?

Kingo za mabawa mawili ya ndege ya abiria huelekea juu. Katika kingo hizi hupakwa rangi kwa kuweka alama ya shirika la ndege, anuani ya tovuti au rangi maalum. Lakini lengo la kuwepo kwa kingo hizi si kuipamba ndege au kulitangaza shirika la ndege.
Katika miongo kadhaa iliyopita viwanda vya ndege vilianza kutengeneza ndege zenye mabawa ambayo kingo zake zinaelekea juu. Lakini abiria wengi hawajawahi kutilia maanani kingo hizi au kufikiri sababu yake.
Ndege inaweza kuruka bila ya kingo hizo, lakini zinatoa mchango katika kuhakikisha usalama wa abiria, kupunguza utoaji wa hewa chafu, na kupunguza kelele.
Katika miaka ya 80 karne iliyopita, kingo hizi zilianza kutengenezwa kwenye ndege za abiria. Boeing 704 ilikuwa ndege ya kwanza yenye kingo hizi. NASA imesema kingo hizi zilianza kutengenezwa kwenye mabawa ya ndege kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta baada ya msukosuko wa mafuta uliotokea mwaka 1973.
Mhandisi wa NASA Bw. Richard Whitcomb alisanifu kingo zinazoelekea juu kwenye mabawa ya ndege katika miaka ya 70 karne iliyopita. Kabla ya hapo, aligundua kuwa ndege wanaporuka, manyoya yaliyoko katika ukingo wa mabawa yao huelekea juu.
Majaribio yamethibitisha kuwa kuweka kingo hizi kunaweza kupunguza asilimia 20 ya vizuizi vya hewa na kubana matumizi ya nishati kwa asilimia 6 hadi 7 bila ya kuongeza uzito wa ndege.
Theluthi moja ya gharama ya uendeshaji wa mashirika ya ndege ni nishati, na kubana matumizi ya nishati kunasaidia kuwapatia abiria tiketi zenye bei nafuu.

0 comments:

Chapisha Maoni