Umoja wa Mataifa umesisitiza juu ya ushiriki zaidi wa wanawake
barani Afrika katika masuala ya kijamii na kisiasa kwa shabaha ya kuleta
amani na uthabiti barani humo.
Phumzile Mlambo-Ngcuka, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja
wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake amesema katika kikao cha
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha umoja huo siku ya Jumatatu
ya jana kwamba, jamii ya kimataifa hususan nchi za Kiafrika zinapaswa
kuwaunga mkono zaidi wanawake na kuipa umuhimu nafasi yao chanya katika
jamii.
Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kwamba, wanawake wana
nafasi muhimu katika kuleta amani na uthabiti barani Afrika, licha ya
kuwa nafasi yao imekuwa ikipuuzwa na kutozingatiwa kama inavyotakiwa.
Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema kuwa, kuanzishwa vituo vya kukabiliana na
migogoro kwa kushirikishwa wanawake lengo likiwa ni kusimamia chaguzi
au kutabiri migogoro ya ndani katika nchi za Kiafrika ni jambo ambalo
daima limekuwa na mafanikio.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake ameongeza kuwa, mazungumzo
na viongozi wa vyama vya kisiasa au maafisa usalama katika nchi zenye
migogoro, hadi sasa yamekuwa na mafanikio.
Mkurugenzi Mtendaji huyo anaeleza hayo katika hali ambayo, wanawake
walioko katika maeneo mbalimbali barani Afrika wamekuwa wakipitia
tajiriba tofauti. Nafasi ya wanawake katika baadhi ya nchi za Kiafrika
ambazo zimepiga hatua kubwa katika uga wa ustawi wa kisiasa na kiuchumi,
nayo imebadilika mno na akthari yao wameingia katika harakati za
kiuchumi na kisiasa.
Katika baadhi ya nchi za Kiafrika kiwango cha
ushiriki wa wanawake katika masuala ya kisiasa kimeongezeka mno. Wengi
wa wanawake hao ni mawaziri au washauri katika serikali na vyama vya
kisiasa huku wengine wengi wakishiriki katika harakti mbalimbali kwenye
asasi zisizo za kiserikali hususan katika kuwasaidia watoto, vitengo vya
elimu na katika vituo vya afya.
Kadhalika katika akthari ya nchi barani
Afrika kutokana na mwenendo wa kiuchumi kupiga hatua, wanawake wengi
wameingia katika uwanja huo kama nguvu kazi na kuwa na nafasi muhimu
katika kudhamini mahitaji ya familia. Pamoja na hayo wanawake barani
Afrika wangali wanakabiliwa na matatizo mengi.
Kustawi utamaduni katika
baadhi ya nchi barani Afrika, kumeshuhudia wanawake katika nchi hizo
wakikabiliwa na dhulma na wengi wao wamekuwa wakinyimwa hata haki zao za
kimsingi kabisa.
Filihali, kuna nchi nyingi barani Afrika ambazo zinakabiliwa na
mapigano ya ndani ya kikabila na kidini. Machafuko yameyafanya mazingira
ya maisha ya wakazi wake hususan wanawake na watoto kuwa mabaya mno.
Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Jamhuri ya Afrika ya
Kati ni baadhi tu ya nchi hizo. Katika nchi ambazo kuna vurugu na
machafuko wanawake na watoto wamekuwa wakikabiliwa na hali mbaya ya
kimwili na kiroho na kukosa huduma muhimu.
Pamoja na matatizo yote hayo,
lakini katika miongo ya hivi karibuni kuna wanawake ambao wamefanikiwa
kubadilisha mazingira yanayowakabili na hivyo kuwa na nafasi muhimu
katika masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi katika nchi husika.
Hivi sasa wanaharakati wengi na asasi za kimataifa zina matumaini
kwamba, katika miaka ijayo ushiriki amilifu wa wanawake katika nyuga za
kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni barani Afrika utakuwa na taathira
chanya katika kupatiwa haki zao na kuondolewa dhulma na uonevu dhidi yao
barani Afrika na kwa muktadha huo kuwaandalia mustakbali mzuri wanawake
hao.
0 comments:
Chapisha Maoni