Jumatatu, Machi 21, 2016

RAIS WA FIFA GIANNI INFANTINO KUZURU RWANDA

Rais mpya wa shirikisho la soka duniani (FIFA) , Gianni Infantino, atafanya ziara nchini Rwanda mwishoni mwa mwaka huu akiwa kwenye ziara yake ya kwanza barani Afrika tangu alipochaguliwa kwa wadhifa huo, hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirikisho la kandanda nchini Rwanda (FERWAFA)
“Nilikuwa mjini Zurich, Uswizi wiki iliyopita nilipokutana na Bw. Infantino na akanihakikishia kuwa Rwanda itakuwa mojawapo ya mataifa atakayotembelea katika ziara yake ya kwanza barani Afrika,” Vincent Nzamwita, rais wa shirikisho la soka nchini Rwanda aliambia maripota. “FIFA imependezwa na ufanisi wa mchezo wa soka nchini Rwanda,” aliongeza Nzamwita.
Gianni Infantino alichaguliwa mwezi uliopita kama rais mpya wa FIFA, na kuchukua nafasi ya Sepp Blatter aliyekuwa akishikila wadhifa huo. Blatter ambaye aliongoza FIFA tangu mwaka wa 1998 alisimamishwa kazi kwa muda wa miaka 6 kwa tuhuma za ufisadi na kukiuka maadili ya shirikisho hilo.
Rwanda inaorodheshwa na FIFA katika nafasi ya 91 kote duniani miongoni mwa mataifa yanayofanya bora zaidi katika kandanda, kati ya mataifa 126 wanachama wa FIFA duniani, na katika nafasi ya 23 miongoni mwa mataifa bora zaidi kwa soka barani Afrika. Katika eneo la Afrika Mashariki, Rwanda wanashikilia nafasi ya pili baada ya Uganda.Burundi wanorodheshwa katika nafasi ya tatu, wakifuatwa na Kenya katika nafasi ya nne, na Tanzania wa tano.

0 comments:

Chapisha Maoni