Jumamosi, Machi 19, 2016

MADINI YA ALMASI YAGUNDULIKA SINGIDA

http://www.2gb.com/sites/default/files/field/image/20160228/unnamed.jpg
Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) wamegundua uwepo wa madini mengi aina ya Almasi pamoja na dhahabu mkoani Singida yanayopatikana katika milima ya Kimbalaiti wilayani Iramba.
Kwa mujibu wa wakala hao ambao ni watafiti wa upatikanaji wa madini nchini na waratibu wa majanga ya asili ya jiolojia, uwepo huo wa madini kunaifanya Kanda ya Kati kushika nafasi ya pili kwa kuwa na madini mengi ukitanguliwa na Kanda ya Ziwa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo, Profesa Abdul Mruma, ameliambia Raia Mwema kuwa madini hayo yamegundulika baada ya upimaji kufanyika kwa kutumia ndege maalumu za kupimia madini chini ya ardhi.
“Tumezoea kuona almasi inapatikana Mwadui mkoani Shinyanga na maeneo ya Kahama, lakini sasa tumeweza kugundua madini ya almasi mengi mkoani Singida yanayopatikana katika milima ya Kimbalaiti wilayani Iramba,” alisema.
Professa Mruma anasema wawekezaji bado hawajahamasishwa vya kutosha ili waweze kujitokeza na kuwekeza kwenye madini yaliyopo kwenye mkoa huo ili uweze kuondokana na umaskini.
Anashauri ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwepo wa madini katika maeneo yao ni vyema Serikali ikatoa leseni kwa wachimbaji wadogo ambao wataweza kuingia ubia na wawekezaji wakubwa ili waweze kupata hisa ambazo zitawalipa vizuri.
‘‘Serikali ikianza kugawa vitalu hivi, mimi ninapendekeza na kuishauri igawe vitalu kwa Watanzania, pia itoe leseni kwa Watanzania ili wao waingie ubia na wawekezaji waweze kupata manufaa zaidi kuliko wawekezaji kuzitajirisha nchi zao,” alisema Professa Mruma.
Alisema wapo wawekezaji ambao hawana utalaamu wa kutosha ambao wamekuwa wakiingia mkataba na wakala wa Jiolojia hao kama washauri, nafasi hiyo pia inaweza kutumiwa na watanzania kuutumia wakala huo katika upimaji.
Wataalam na wananchi wameonya kuwa kuwepo kwa madini ya aina tofauti katika mkoa wa Singida huku mengine kama ya almasi yakiendelea kugundulika yanaweza yasilete tija kwa wananchi husika iwapo Serikali haitaweka utaratibu mzuri.
Wameonya kuwa ugunduzi huo lazima kujiepusha na makosa yaliyofanyika katika kijiji cha Nyakabale mkoani Geita ambao wanazungukwa na mgodi wa dhahabu wa Geita lakini umaskini umetamalaki kwa wananchi hao.

0 comments:

Chapisha Maoni