Wananchi wa Zanzibar kesho Jumapili wanatazamiwa kuelekea kwenye
masanduku ya kupiga kura katika uchaguzi wa marudio visiwani humo, ambao
utashirikisha wagombea wa urais na wagombea wa ujumbe wa Baraza la
Wawakilishi kutoka vyama mbalimbali.
Wakati maandalizi yakiwa katika hatua za mwisho, Umoja wa Vijana
wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM, umesema uchaguzi wa marudio utakaofanyika
kesho visiwani humo, ndiyo utakaotatua na kuhitimisha mvutano wa kisiasa
ulioripuka baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC kufuta matokeo ya
uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana. Umoja huo umewataka vijana pamoja na
Wazanzibari wote kujitokeza kwa wingi kupiga kura, ili kutumia haki yao
ya kuchagua rais kukwamua mzozo wa kisiasa visiwani Zanzibar. Kaimu
Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka alisema hayo jana alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi Kuu ya UVCCM, Gymkhana
mjini Unguja. Shaka alisema wale wanaosema Zanzibar kuna mgogoro au
tatizo linalohitaji kupatiwa suluhu, hawajatambua kiini cha tatizo na
ufumbuzi wake. Alisema kiini cha tatizo linalosababisha mivutano ya
kisiasa, ni Chama cha Wananchi (CUF) kukaidi utii wa matakwa ya sheria
na kutaka kupuuza Katiba ya Zanzibar. Tayari ZEC imeshakamilisha hatua
za msingi za kufanyika kwa uchaguzi huo, ikiwemo kuwasili kwa karatasi
za kura. Hii ni katika hali ambayo, vyama tisa kati ya 14 vilivyoshiriki
katika uchaguzi uliofutwa wa Oktoba 25, kikiwemo Chama cha Wananchi CUF
ambacho kinadai mgombea wake wa urais Maalim Seif Sharif Hamad ndiye
mshindi halali wa kiti hicho, vikiwa vimeshatangaza rasmi kwamba,
havitashiriki katika uchaguzi huo.
0 comments:
Chapisha Maoni