Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi ameteuliwa kuongoza timu ya waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda wa Februari 18.
Kwa mujibu wa taarifa ya sekritariati ya EAC, timu hiyo imepewa majukumu ya kufuatilia mazingira ya uchaguzi, harakati za kabla ya uchaguzi, uchaguzi wenyewe na kufuatilia kwa karibu zoezi la kuhesabu kura.
Wanachama wa timu hiyo wameteuliwa kutoka nchi 5 wanachama wa EAC ambazo ni Tanzania, Kenya, Burundi, Uganda na Rwanda; wabunge kadhaa wa Bunge la Afrika Mashariki, Kundi la Vijana wa jumuiya hiyo na maafisa kadhaa kutoka makao makuu ya jumuiya hiyo mjini Arusha, Tanzania.
Huku hayo yakijiri, Umoja wa Afrika nao umetangaza kuwa utatuma waangalizi wa uchaguzi kufuatilia zoezi la upigaji kura nchini Uganda. Taarifa ya umoja huo imesema kuwa waangalizi hao watafuatilia kwa makini chaguzi za rais, bunge na serikali za mitaa na umeitaka serikali ya Kampala na wasimamizi wa uchaguzi kutoa ushirikiano kwa waangalizi hao. AU imesema itatuma nchini Uganda timu ya watu 40 itakayoongozwa na Bi. Sofia Okofor kutoka Mahakama ya Kilele ya Ghana kuanzia hapo kesho na kwamba ujumbe huo utabakia Uganda hadi Februari 22.
Uchaguzi mkuu wa Uganda unatarajiwa kufanyika Februari 18 na kiti cha urais kimewavutia wagombea 8 akiwemo Rais wa sasa, Yoweri Museveni. Hata hivyo mchuano mkali kwenye kiti cha urais unatarajiwa kuwa kati ya Museveni, Daktari Kizza Besigye wa chama cha FDC pamoja na Waziri Mkuu wa zamani, Amama Mbabazi ambaye anawania nafasi hiyo kama mgombea binafsi.
0 comments:
Chapisha Maoni