Jumapili, Januari 31, 2016

WATALIANO WAPINGA KUHALALISHWA NDOA ZA JINSIA MOJA

Makumi ya maelfu ya watu kutoka miji mbalimbali nchini Italia wameandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo, Roma kupinga mpango wa serikali wa kutaka kuhalalisha kisheria ndoa za watu wa jinsia moja.
Waandamanaji hao walikusanyika jana katika moja ya maeneo makuu ya kale la Circus Maximus mjini Roma wakitaka kufutwa uamuzi wa kuujadili mpango huo wa serikali katika bunge la nchi hiyo.
Mpango huo ambao uliwasilishwa bungeni wiki iliyopita na unatazamiwa kupigiwa kura na bunge mwezi ujao wa Februari umesababisha mpasuko mkubwa ndani ya serikali ya nchi hiyo. Mpango huo unaruhusu watu wa jinsia moja kuwa na mahusiano ya kindoa na kuwa na mamlaka ya kuasilisha mtoto. Simone Pillon, mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo amesema:"Tunataka sheria hii ifutwe kikamilifu bila ya hili wala lile".
Franco Pantuso, mwenye umri wa 71, ambaye alikuwa mmoja wa waandamanaji amesema:"Sheria hii inapingana na Mungu na inapingana na Biblia; mimi ni babu, lazima watoto wetu na wajukuu zetu walindwe".
Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki alitoa angalizo kali la upinzani wa Kanisa dhidi ya ndoa za watu wa jinsia moja aliposisitiza kuwa familia ya jadi ni "familia anayoitaka Mungu".

0 comments:

Chapisha Maoni