Jumatatu, Januari 25, 2016

WARUNDI NA WACHINA WAONGOZA KATIKA IDADI YA WAHAJIRI HARAMU TANZANIA

Operesheni ya kukamata raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini Tanzania bila ya kuwa na vibali imebaini kuwa, China na Burundi zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wahamiaji haramu wanaoishi nchini ikilinganishwa na nchi nyingine.
Tangu kuanza kwa operesheni hizo mwezi Desemba mwaka jana hadi katikati ya mwezi huu, idadi ya raia wa kigeni wasiokuwa na vibali waliokamatwa; kutoka China walikuwa ni 285, Burundi 284, wakifuatia 157 wa Ethiopia.
Raia wengine waliokamatwa na polisi ya Tanzania ni kutoka India 41, Zambia 40, Kongo DR 34, Malawi 27, Kenya 26, Uganda 13, Ivory Coast 10, Korea tisa, Nigeria wanane, Somalia saba, Madagascar watano, Rwanda watatu, Lebanon mmoja, Zimbabwe mmoja, Ghana na Afrika Kusini mmoja na wengine 11 uraia wao bado una utata.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania, Charles Kitwanga akizungumza katika sherehe za mwaka mpya wa China jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii alisema kuwa, kati ya watu hao waliotiwa mbaroni, baadhi wamepelekwa katika kambi za wakimbizi, hasa raia waliotoka Burundi, wengine wamepewa amri ya kuondoka nchini na wengine kesi zao ziko katika hatua mbalimbali mahakamani.
Aidha ameongeza kuwa, operesheni hiyo ya kukamata raia wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini bila vibali haitawagusa wenye vibali halali. Kitwanga alisema wizara yake imetoa vibali vya ukazi kwa wageni 40,765 kutoka mataifa mbalimbali kati ya mwaka 2014 na Januari mwaka huu na kwamba idadi hiyo inaendelea kuongezeka siku hadi siku.

0 comments:

Chapisha Maoni