Waislamu nchini Tanzania wameaswa kutunza amani ya nchi kwa kuendelea kutenda mema na kujiepusha na vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani katika jamii. Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam, na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Wakfu wa Imamu Bukhari.
Shekh Khalifa Khamisi ameyasema hayo wakati wa warsha iliyowakutanisha Waislamu wa matabaka na madhehebu mbalimbali jijini Dar es Salaam, lengo lake likiwa ni kujadili changomoto zinazowakabili Waislamu nchini humo na duniani kwa ujumla.
Sheikh Khalifa Khamis amesema, kuna baadhi ya waislamu wamekuwa wakifanya mambo ya kumkera Mwenyezi Mungu kwa kuwafanyia wenzao mambo maovu, jambo ambalo amesema haliendani na mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.
Amesema, Uislamu unawafundisha wafuasi wake kuwapenda watu wote ndani ya jamii, kusaidiana, kuelekezana na kufanya mambo ya maendeleo.
Amefafanua kuwa, kwa sasa watu wengi wamekuwa wakiyahusisha masuala ya ugaidi yanayotokea duniani na dini ya Kiislamu, jambo ambalo amelipinga na kusema watu wanaofanya vitendo hivyo si Waislamu halisi kwani dini hiyo haina uhusiano wowote na vitendo vyao vya kigaidi.
Kwa upande wake Shekh Hemed Jalala, Mkuu wa Hawza ya Imam Sadiq ya jijini Dar es Salaam Tanzania ambaye naye alikuwa mchangia mada katika semina hiyo, amewaasa Waislamu kuendeleza kufanya mambo mema yatakayomfurahisha Mtume Muhammad (SAW) kwa kusema ndio njia pekee ya kupata mafanikio ya duniani na Akhera.
0 comments:
Chapisha Maoni