Alhamisi, Januari 07, 2016

US: TUNA SHAKA NA BOMU LA HYDROGEN LA PYONGYANG

Huku Marekani ikitilia shaka bomu la hydrogen ambalo lilifanyiwa majaribio hapo jana na Korea Kaskazini, Umoja wa Mataifa umetishia kuiwekea vikwazo serikali ya Pyongyang kwa hatua yake hiyo.
Msemaji wa Ikulu ya White House ya Marekani, Josh Earnest amesema tathmini iliyofanywa na Washington haiambatani na madai ya Pyongyang ya kufanikiwa katika kulifanyia jaribio bomu hilo lenye uwezo mkubwa. 
Rais Barack Obama wa Marekani anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na Rais wa Korea Kusini Park Geun-Hye ambao wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na hatua ya Korea Kaskazini kulifanyia majaribio bomu hilo. Korea Kaskazini jana ilitoa taarifa na kusema imefanya jaribio lake la kwanza kabisa la bomu la hygrogeni. 
Taarifa hiyo iliyosambazwa na Shirika Rasmi la Habari la Korea Kaskazini imesema kuwa, nchi hiyo imeweza kufanya majaribio ya bomu la hydrogeni. Hii ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kuchukua hatua hiyo baada ya tangazo lake la mwaka jana kuwa imepata teknolojia ya kutengeneza bomu la hydrogeni ambalo lina nguvu mara kadhaa zaidi ya bomu la atomiki. 
Bomu la hydrogeni lina uwezo wa kusababisha uharibifu mkubwa zaidi kuliko bomu la atomiki na linapolipuliwa huwa na nguvu za mabomu kadhaa kutokana na izotopu za hydrogeni. Jaribio hilo lilipelekea kuibuka mtetemeko mkubwa wa ardhi lenye ukubwa wa 5.1 kwenye kipimo cha rishta.

0 comments:

Chapisha Maoni