Alhamisi, Januari 28, 2016

KUTOKA IDARA YA UHAMIAJI

IDARA ya Uhamiaji inapenda kuwataarifu Wananchi na Wadau wote wa huduma za uhamiaji kama ifuatavyo;
1. Idara ya Uhamiaji hapo awali ilikuwa ikitoa hati iliyojulikana kama “Carrying On Temporary Assignment Pass” maarufu kama CTA,ili kuwawezesha Raia wa kigeni wanaoingia nchini kwa shughuli za muda mfupi kufanya shughuli zao. Utoaji wa CTA ulisitishwa tarehe 16 Desemba 2015, baada ya kubainika changamoto za kiutendaji ikiwemo ukiukwaji wa Taratibu za Utoaji wa Hati hiyo na hata matumizi yake.
2. Baada ya kusitishwa utoaji wa CTA, zilijitokeza changamoto mbali mbali ambazo kwa kiasi zilisababisha usumbufu kwaRaia wa kigeni ambao waliingia au walikuwa wanataka kuingia nchini kwa shughuli za muda mfupi “Short Term Business Activities”.
3. Idara ya Uhamiaji inapenda kuwafahamisha Wananchi na Wadau wa huduma za uhamiaji kuwa, tokea mwezi Machi 2015 ilikwishaanza mchakato wa kurekebisha Kanuni za Uhamiaji za mwaka 1997, kwa lengo la kufanyiakazi changamoto zilizojitokeza katika utoaji wa CTA. Tayari marekebisho ya Kanuni hizo yamekwishasainiwa na Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na taratibu za kuzitangaza katika Gazeti la Serikali zinaendelea ikiwemo kupitisha Kanuni zinazosimamia utoaji wa Visa (Visa Regulations).
4. Kwa taarifa hii, Idara ya Uhamiaji inapenda kuwafahamisha wananchi na wadau wa huduma za Uhamiaji na Raia wa kigeni wanaotakakuingia nchini kwa shughuli za muda mfupi kuwa Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mamlaka aliyonayo kupitia kifungu cha 33 cha Sheria ya Uhamiaji Na. 7 ya mwaka 1995 (Sura ya 54 Rejeo la 2002) ameidhinisha Idara ya Uhamiaji kuanza kutoa Business Visa kwa ada ya dola za Kimarekani mia mbili na hamsini (USD 250), na Business Pass kwa ada ya Dola za Kimarekani mia mbili (USD 200), kuanzia tarehe 15 Januari, 2016 wakati utaratibu wa kurasimisha utoaji wa hati hizi katika Kanuni unaendelea.
5. Hati hizi “Business Visa na Business Pass” zitatolewa kwa idhini ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kupitia mamlaka zifuatazo;
i. Ofisi ya Uhamiaji Makao Makuu
ii. Ofisi ya Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar
iii. Vituo vya Uhamiaji vya kuingilia nchini “Entry Points”
iv. Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nje ya nchi (Tanzania Missions Abroad).
6. “Business Visa” itatolewa kwa wa siku tisini (90), kwa raia wa kigeni wanaotoka katika nchi ambazo raia wake wanahitaji Visa kuingia nchini na haitaongezwa muda.
7. “Business Pass” itatolewa kwa muda wa siku tisini (90), kwa raia wa kigeni wanaotoka katika nchi ambazo raia wake hawahitaji Visa kuingia nchini na haitaongezwa muda.
8. “Business Visa na Business Pass” hazitatolewa kwa raia wa kigeni wanaokuja nchini kwa madhumuni ya kupata ajira, kwani wageni wa aina hiiyo wanapaswa kabla ya kuajiriwa kuomba kibali cha Kazi kutoka Idara ya Kazi.

0 comments:

Chapisha Maoni