Jumatano, Oktoba 01, 2014

TAREHE YA LEO KATIKA HISTORIA

Miaka 29 iliyopita sawa na siku kama ya leo ya tarehe Mosi Oktoba mwaka 1985 ndege za kijeshi za utawala haramu wa Israel ziliyashambulia makao ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) huko Tunisia. Watu wapatao 70 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa kufuatia mashambulio hayo. PLO ilikuwa imehamishia makao yake Tunisia kutoka Lebanon baada ya mashambulio ya kijeshi ya utawala haramu wa Israel nchini humo mwaka 1982. Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo ulilifanya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lishindwe kuchukua hatua zozote za maana dhidi ya Tel Aviv.
Na Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, nchi ya Nigeria ilipata uhuru. Wareno waliwasili Nigeria katika karne ya 15 na mkoloni Mwingereza naye akawasili katika nchi hiyo katika karne ya 16. Katika karne ya 17 ardhi ya Nigeria iligeuzwa na kuwa moja kati ya vituo muhimu vya biashara ya utumwa. Mwishoni mwa karne ya 19 vikosi vya jeshi la Uingereza viliidhibiti kikamilifu ardhi ya Nigeria. Mwaka 1914 Uingereza iliziunganisha nchi mbili za Nigeria ya Kaskazini na Kusini zilizokuwa chini ya udhibiti wake na kuunda koloni moja la Nigeria. Miaka 40 baadaye nchi hiyo ilijitangazia  utawala wa ndani. Hatimaye baada ya kupitia misukosuko mingi, Nigeria ilipata uhuru katika siku kama hii ya leo.

0 comments:

Chapisha Maoni