Mtu mmoja mkazi wa Itewe wilaya ya Mbeya Vijijini
aliyefahamika kwa jina la Jacob Kimaila (31) ameuawa baada ya kupigwa na kundi
la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkononi kutokana na tuhuma za kuvunja
duka, salon na kuiba.
Mtuhumiwa alifariki mnamo tarehe 05.10.2014 majira ya saa
09:30 asubuhi huko katika kituo cha afya Inyala, kata ya Inyala, tarafa ya Tembela, wilaya ya Mbeya vijijini, mkoa wa Mbeya. Inadaiwa kuwa, chanzo cha
kifo chake ni kutokana na majeraha
aliyoyapata kutokana na kupigwa na wananchi siku ya tarehe 04.10.2014 majira ya
asubuhi.
Jitihada za kuwatafuta waliohusika katika tukio hili
zinaendelea. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya Inyala
alipokuwa anapatiwa matibabu.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishina msaidizi
mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya
kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na badala yake
wawafikishe katika mamlaka husika watuhumiwa wanaowakamata kwa tuhuma
mbalimbali kwa hatua zaidi za kisheria.
0 comments:
Chapisha Maoni